Mkuu wa IAEA: Iran inataka kuona dunia yenye usalama na uthabiti
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) amesema hamu kubwa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuona usalama na uthabiti vinatawala duniani kote, na kwamba Tehran iko tayari kufanya mazungumzo amilifu na mataifa ambayo yapo tayari kufuata njia ya mazungumzo.
Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA alisema hayo jana Jumatano katika mahojiano na televisheni ya CBS News ambapo pia amekosoa hatua ya Marekani ya kujiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Ameeleza bayana kuwa: Iran inaendelea na miradi yake ya nyuklia. Kama unavyojua, hili halifanyika katika ombwe, bali linafanyika katika fremu ya makubaliano, yaliyosainiwa na kundi la P5 (Nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambazo ni Marekani, Uingereza, Ufaransa, China na Russia), pamoja na Ujerumani na Umoja wa Ulaya (EU) mwaka 2015.
Grossi amesisitiza kuwa, baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano hayo mwaka 2018, Iran ilianza kupunguza uwajibikaji wake kwenye makubaliano hayo kama jibu kwa hatua hiyo ya Washington. Mkurugenzi Mkuu wa IAEA amebainisha kuwa, mustakabali wa JCPOA unategemea maamuzi yatakayochukuliwa na nchi washiriki wa mapatano hayo katika kipindi cha wiki na miezi kadhaa ijayo.

Hivi karibuni pia, Grossi alikiri kuwa, kinyume na inavyodai Marekani, mpango wa nyuklia wa Iran unafuatilia malengo ya amani.
Katika mahojiano na gazeti la Die Presse la Austria, Grossi alitupilia mbali madai yasiyo na msingi ya Wamarekani na Wazayuin kuwa eti Iran inalenga kuunda bomu la atomiki na kusisitiza kuwa, Iran haijatengeneza mada zinazotosha kuunda bomu la atomiki.