Waliouawa na wanajeshi katika maandamano ya Myanmar wapindukia 500
https://parstoday.ir/sw/news/world-i68462-waliouawa_na_wanajeshi_katika_maandamano_ya_myanmar_wapindukia_500
Shirika moja la kiraia nchini Myanmar limesema idadi ya watu waliouawa katika maandamano ya wananchi ya kupinga utawala wa kijeshi nchini humo ni zaidi ya watu 500.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 30, 2021 08:12 UTC
  • Waliouawa na wanajeshi katika maandamano ya Myanmar wapindukia 500

Shirika moja la kiraia nchini Myanmar limesema idadi ya watu waliouawa katika maandamano ya wananchi ya kupinga utawala wa kijeshi nchini humo ni zaidi ya watu 500.

Jumuiya ya Wafungwa wa Kisiasa nchini humo (AAPP) leo Jumanne imesema kuwa imethibitisha vifo vya raia 510 katika maandamano hayo, na kwamba yumkini idadi hiyo ikawa ya juu zaidi.

Siku ya Jumamosi, wanajeshi na polisi waliwakandamiza waandamanaji na kusababisha idadi kubwa zaidi ya watu kufa kwa siku moja tangu maandamano yalipoanza mwezi uliopita. Raia 107 wakiwemo watoto wadogo saba waliuawa katika maandamano hayo.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres katika kikao na waandishi wa habari ameitaka jamii ya kimataifa ichukue hatua za kulishinikiza jeshi la Myanmar, ili kuhakikisha kuwa mauaji hayo ya kikatili ya raia wa nchi hiyo yanakomeshwa.

Huku hayo yakiarifiwa, duru za kidiplomasia zimearifu kuwa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kufanya mkutano wa dharura kesho Jumatano kujadili hali ya Myanmar.

Maandamano ya wananchi wa Myanmar wakipinga utawala wa kijeshi

Jeshi la Myanmar lilitwaa madaraka ya nchi Februari Mosi baada ya kumkamata Rais wa nchi hiyo, Win Myint na viongozi wengine akiwemo Aung San Suu Kyi, kiongozi wa chama tawala mwenye ushawishi mkubwa, kufuatia siku kadhaa za mivutano nchini humo.

Kisingizio cha jeshi cha kufanya mapinduzi hayo ni madai yake ya kutokea wizi na udanganyifu katika zoezi la uchaguzi wa Bunge wa Novemba mwaka jana (2020), ambapo kwa mujibu wa matokeo, chama tawala cha National League for Democracy (NLD) kinachoongozwa na Aung San Suu Kyi kiliibuka na ushindi.