Apr 11, 2023 11:51 UTC
  • Helikopta na ndege kivita za jeshi la Myanmar zashambulia na kuua makumi ya watu

Jeshi la Myanmar limefanya mashambulizi ya anga katika mji wa kati mwa nchi hiyo unaojulikana kuwa ngome ya upinzani dhidi ya mapinduzi yaliyofanywa na jeshi hilo miaka miwili iliyopita.

Mashuhuda na vyombo vya habari vya ndani vimesema makumi ya watu wameuawa na kujeruhiwa katika shambulio hilo la leo, ambalo ni moja ya mashambulio mabaya zaidi kufanywa na jeshi hilo tangu liliponyakua hatamu za utawala.

Zikiwanukuu wakazi wa Sagaing, mji uliopo yapata kilomita 110 (maili 45) magharibi mwa jiji kuu la Yangon, ripoti za habari zimesema, takriban watu wasiopungua 30 wakiwemo raia wameuawa katika shambulio hilo lililolenga mji wa Pazigyi.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, mashambulizi hayo ya anga yalifanywa wakati wakazi wa mji huo walipokusanyika kwa ajili ya uzinduzi wa ofisi ya utawala.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa, saa moja na nusu leo asubuhi umati wa watu ulishambuliwa na ndege za kivita zilizofuatiwa na helikopta aina ya Mi-35. 

Watu 40 wamethibitishwa kufariki dunia lakini vyombo vya habari vinashuku idadi ya vifo itaongezeka sana kutokana na ukubwa wa shambulio hilo baya, ambalo limeelezwa kuwa limewalenga zaidi raia.

Jeshi la Myanmar limeshutumiwa kwa mauaji ya kiholela ya raia huku likishiriki katika mashambulizi makubwa kukandamiza upinzani wa silaha unaopinga unyakuzi wake wa madaraka kutoka utawala wa raia.../

Tags