Oct 18, 2023 03:51 UTC
  • UN: Migogoro mingine isifanye wakimbizi Warohingya wasahaulike

Kamishna Mkuu wa Wakimbizi wa Umoja wa Mataifa ameitaka jamii ya kimataifa isishugulishwe tu na migogoro mipya na kuwasahau wakimbizi Waislamu Warohingya wa Myanmar.

Filippo Grandi alitoa a mwito huo jana Jumanne na kusisitiza kuwa, misaada zaidi inahitajika ili kuwasaidia Warohingya na kuzisaidia nchi zilizolemewa na mzigo wa wakimbizi hao wa Myanmar.

Grandi alitoa mwito huo jana pambizoni mwa mkutano wa kieneo wa kujadili hali ya wakimbizi wa Warohingya, uliofanyika Bangkok, na kuhudhuriwa na wajumbe kutoka Thailand, Bangladesh, India, Indonesia, Malaysia, Uingereza na Marekani.

Kamishna Mkuu wa Wakimbizi wa Umoja wa Mataifa ametaka hatua zaidi zichukuliwe kimataifa ili kuondokana na janga hilo linalokumba Warohingya, na wale wanaotekeleza ukatili dhidi yao wafikishwe mbele ya sheria. 

Kwa mujibu wa Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, zaidi ya Warohingya milioni moja wamekimbia mateso sambamba na mfumo wa ubaguzi na hivyo wamesaka hifadhi katika nchi jirani ya Bangladesh. Aidha zaidi ya warohingya 100,000 wanaishi kwenye makazi ya wakimbizi nchini Myanmar.

Wakimbizi Waislamu wa Rohingya

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu ilisema, jeshi la Myanmar liliongeza ukandamizaji wake kwa mauaji ya watu wengi, mashambulizi ya anga na mizinga katika kipindi cha mwaka uliopita wakati likipambana kuzima upinzani dhidi ya wanaopinga mapinduzi yake nchini Myanmar.

Jeshi la Myanmar lilitwaa madaraka ya nchi Februari mwaka 2021 baada ya kumkamata Rais wa nchi, Win Myint na viongozi wengine akiwemo Aung San Suu Kyi, kiongozi wa chama tawala mwenye ushawishi mkubwa, kufuatia siku kadhaa za mivutano nchini humo. Tangu wakati huo hadi sasa, serikali ya kijeshi ya Myanmar imeshindwa kutuliza hali ya mambo na upinzani dhidi yake unaendelea, sambamba na mauaji ya raia.

Tags