Jun 27, 2024 12:25 UTC
  • Kuongezeka kasi katika ushirikiano wa kimkakati kati ya Iran na Russia

Uhusiano na ushirikiano wa kistratijia kati ya Iran na Russia umeongezeka na kushika kasi zaidi katika siku za hivi karibuni, na sasa unaingia katika hatua mpya.

Hafla ya kusainiwa makubaliano ya kimkakati kati ya Kampuni ya Taifa ya Gesi na Gazprom ya Russia imefanyika Jumatano wiki mbele ya Mohammad Mokhber, Kaimu Rais wa Jamhuri ya Kislamu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Gazprom ya Russsia, Alexey Miller katika Ofisi ya Rais mjini Tehran.

Kaimu Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika mazungumzo yake ya simu na Rais Vladimir Putin wa Russia kwamba kutiwa saini mapatano ya kusafirisha gesi ya Russia hadi Iran ni hatua muhimu katika mwelekeo wa kuimarisha uhusiano wa nchi mbili na hatua athirifu inayolenga kustawisha uchumi wa kanda hii. Mohammad Mokhber amesema, kutekelezwa mpango huo, sio tu kwamba kutadhamini maslahi ya kiuchumi ya nchi mbili, bali maslahi ya kanda nzima. Vilevile ameshukuru juhudi za Rais wa Russia katika kufanikisha makubaliano hayo.

Akielezea kuridhishwa kwake na maendeleo ya utekelezwaji wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Tehran na Moscow, Mokhber amesema uhusiano wa kistratijia wa pande mbili hautabadilika. Amesisitiza umuhimu wa mazungumzo na mtazamo wa pamoja wa Iran na Russia kuhusu masuala ya kieneo, na kuelezea matumaini yake kuwa juhudi za nchi mbili za kuimarisha utulivu zitazaa matunda yanayotarajiwa.

Kwa upande wake, Rais Vladimir Putin, pia ameeleza kuridhishwa na kutiwa saini makubaliano ya pamoja ya kimkakati ya usafirishaji gesi kati ya Russia na Iran na kuyataja makubaliano hayo kuwa ni tukio muhimu kwa ajili ya kulinda maslahi ya nchi hizo na kuimarisha ushirikiano wa pande mbili kwa manufaa ya masoko ya kikanda na kimataifa. Rais Putin ameeleza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imethibitisha kwamba ushirikiano wa pande mbili haubaki kwenye karatasi na unafikia hatua ya utekelezaji. Amepongeza bidii na umakini wa serikali ya Shahid Ebrahim Raisi katika kustawisha na kutekeleza makubaliano kati ya nchi hizo mbili na amewatakia watu wa Iran mafanikio na ufanisi katika uchaguzi ujao wa rais.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mafuta wa Iran, makubaliano haya ni hatua inayofuatia makubaliano ya mwaka jana kati ya Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Iran na kampuni ya Gazprom ya Russia, na yanaonyesha kuwa makubaliano hayo yanaelekea kwenye utekelezaji. Kwa makubaliano haya, sehemu ya biashara ya Iran inapaa juu zaidi na kubadilisha mizani ya kimataifa katika sekta hiyo. Makubaliano ya gesi kati ya Iran na Russia pia yanatambuliwa kama mapinduzi katika uwanja wa nishati na viwanda katika kanda hii.

Wakati huo huo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Maria Zakharova, alisema kuwa Moscow inafanyia kazi mkataba mkubwa na Iran. Kauli hiyo ya Zakharova imetolewa huku Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Rudenko Andrey Yurevich akisema siku ya Jumanne kwamba: "Moscow inatarajia kutia saini mkataba wa ushirikiano wa pande zote na Iran katika siku za usoni."

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ilitangaza mwezi Januari kwamba mkataba mpya kati ya Moscow na Tehran uko katika hatua za mwisho na utaakisi ongezeko kubwa lisilo na kifani la uhusiano kati ya Russia na Iran.

Makubaliano hayo makubwa na mapya kati ya Moscow na Tehran yalifikiwa Septemba 2022 wakati wa mkutano kati ya Rais wa Russia, Vladimir Putin, na Rais wa Iran, Ebrahim Raisi.

Russia na Iran zimepanua uhusiano wao katika miaka ya hivi karibuni, hasa baada ya kuja madarakani Serikali ya Awamu ya 13 nchini Iran na kuanza mashambulizi ya Moscow dhidi ya Ukraine Februari 2022. Tangu mwanzo mwa karne mpya, nchi hizo mbili zimetilia mkazo ushirikiano wa kimkakati. Wakati huo huo, kunashuhudiwa vichochezi mbalimbali vinavyotayarisha njia ya kutekelezwa makubaliano ya kistratijia kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia. Vishawishi hivyo ni pamoja na masuala ya kihistoria, kisiasa, n.k, na hapana shaka kuwa kuzingatiwa kwake kunaweza kuimarisha nia na irada ya pande mbili ya kutekelezwa makubaliano hayo.

Uelewa na mitazamo ya pamoja ya Iran na Russia kuhusu vyanzo vya vitisho vya kitaifa, kieneo na kimataifa, vikiwemo vitisho kama vile sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Marekani, ukiukaji wa sheria za kimataifa, ubabe wa serikali ya Washington na misimamo ya kindumakuwili ya madola ya Magharibi katika sera za kigeni vinetia msukumo mkubwa katika harakati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Serikali ya Shirikisho la Russia ya kufikia makubaliano ya kimkakati ya muda mrefu.