Jun 29, 2024 07:20 UTC
  • Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan
    Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan

Mkuu wa Baraza la Utawala na Kamanda wa Jeshi la Sudan, Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan, anakaribia kumtangaza waziri mkuu mpya atakayeunda serikali ya kitaifa.

Duru za Sudan zinasema kuwa Al Bashir amekutana na vyama na makundi tofauti ya kisiasa ya Sudan huko Port Sudan, mji mkuu wa muda, kwa ajili ya kushauriana juu ya suala hilo. 

Ripoti zinasema, Al-Burhan amewafahamisha viongozi wa kisiasa kuhusu nia yake ya kutangaza waziri mkuu mpya ndani ya wiki mbili zijazo, na kumpa jukumu la kuunda serikali ya kitaifa yenye mamlaka kamili ya kusimamia nchi hadi mkutano wa mazungumzo ya Wasudani utakapofanyika kujadili na kukubaliana juu ya kipindi cha baada ya vita na jinsi ya kukabiliana na changamoto za ndani na nje.

Vyanzo vya ndani vimeripoti kuwa mkutano wa Al-Burhan na viongozi wa kisiasa pia umejadili mkutano ulioitishwa na Misri baina ya wawakilishi wa vyama vya siasa na makundi ya kiraia mnamo Julai 6 huko Cairo ili kujadili suluhisho la mzozo wa Sudan.

Itakumbukwa kuwa, Kamanda wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RFS), Mohamed Hamdan Dagalo alitishia mwezi Septemba mwaka jana kwamba iwapo Al-Burhan ataunda serikali huko Port Sudan, ataanza mashauriano ya kuunda serikali katika maeneo anayodhibiti, mji wake mkuu ukiwa  Khartoum.

Dagalo na al Burhan

Dagalo ambaye vikosi vyake vinapigana na jeshi la taifa la Sudan, alisema hataruhusu kuundwa mji mkuu mwingine badala ya Khartoum.