Taasisi 27 za Marekani zamtaka Biden apunguze mizozo na Russia
Taasisi 27 za nchini Marekani zimemtaka rais wa nchi hiyo, Joe Biden ajiepushe na kushadidisha mivutano na misuguano na Russia.
Hayo yameripotiwa na mtandao wa habari wa The Hill wa nchini Marekani ambao umeongeza kuwa, taasisi 27 za nchi hiyo zimetoa tamko la pamoja na kumtaka Joe Biden ajiepushe na kutoa matamshi ya kumvunjia heshima Rais Vladmir Putin wa Russia kwani hakuna matunda yoyote isipokuwa kuongezeka mivutano na ugomvi tu baina ya nchi hizo mbili.
Ikumbukwe kuwa, hivi karibuni uhusiano wa Marekani na Russia uliingia kwenye mzozo mkubwa baada ya rais wa Marekani, Joe Biden kumshambulia kwa maneno Rais Vladimir Putin wa Russia kwa kumwita muuaji.
Katika mahojiano na televisheni ya ABC News, Biden alitoa tuhuma nzito dhidi ya rais wa Russia na kusema kuwa Vladimir Putin atalipa gharama kubwa kwa kuingilia uchaguzi wa Marekani. Akijibu swali la mwandishi habari aliyemuuliza, je unamjua Vladimir Putin? Unadhani kwamba yeye ni muuaji? Joe Biden alijibu kwa kusema: "Nadhani kwamba ni muuaji." Biden alimtuhumu pia Putin kwamba alifanya njama za kumchafulia jina wakati wa uchaguzi wa hivi karibuni wa Marekani.
Moscow ilimwita nyumbani balozi wake mjini Washington na kusema kwamba inashangaza kuwaona viongozi wa Marekani ambao ni wauaji wakubwa, wakiwatuhumu watu wengine kwa mauaji. Akijibu tuhuma hizo za rais wa Marekani, Rais Vladimir Putin wa Russia alisema, mkitaka kumjua muuaji, basi ni huyo anayewatuhumu wengine kuwa ni wauaji.