Ripoti: Watu milioni 40 ni wakimbizi katika nchi zao
Watu zaidi ya milioni 40 katika nchi mbali mbali duniani wamelazimika kuwa wakimbizi wa ndani ya nchi kutokana na vita na migogoro.
Kwa mujibu wa shirika moja la misaada ya kibidamu la Internal Displacement Monitoring Center (IDMC), watu milioni 40 na laki 8 walilazimika kuwa wakimbizi ndani ya nchi zao kufikia mwishoni mwa mwaka jana wa 2015.
Ripoti ya shirika hilo iliyotolewa jana Jumatano imesema kuwa, watu milioni 8.6 miongoni mwao walifurushwa kutoka kwenye nyumba zao ndani ya nchi zao mwaka jana.
Uchunguzi wa Internal Displacement Monitoring Center (IDMC) umebainisha kuwa, kwa wastani watu 24,000 hulazimika kuwa wakimbizi katika nchi zao kila siku, huku asilimia 50 ya visa hivyo vikiripotiwa katika nchi za Syria, Iraq na Yemen.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, watu milioni 2.2 wamelazimika kuwa wakimbizi nchini Yemen tangu Machi mwaka jana 2015, baada ya Saudi Arabia na waitifaki wake kuanzisha mashambulizi ya anga dhidi ya nchi hizo eti kwa lengo la kumrejesha madarakani rais mtoro wa nchi hiyo Abd Rabbu Mansur Hadi.
Mbali na Mashariki ya kati, nchi zingine ambazo zina idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani ya nchi ni Afghanistan, Jamhuri ya Afika ya Kati, Colombia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Nigeria, Sudan Kusini na Ukraine.
kwa mujibu wa ripoti ya IDMC, watu milioni 19.2 wamelamizika kuyahama makazi yao na kuwa wakimbizi ndani ya nchi kutokana na sababu za kimaumbile kufikia mwishoni mwa mwaka jana 2015.