Aliyekuwa muigizaji wa Bollywood awajibu wanaomdhihaki kwa kuvaa Hijabu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i70864-aliyekuwa_muigizaji_wa_bollywood_awajibu_wanaomdhihaki_kwa_kuvaa_hijabu
Muigizaji mashuhuri wa zamani wa sekta ya filamu ya Bollywood ya India amewajia juu watumiaji wa mitandao ya kijamii wanaomdhihaki na kumkejeli kwa kuvaa vazi la stara la Hijabu.
(last modified 2024-06-10T09:25:34+00:00 )
Jun 04, 2021 02:40 UTC
  • Sana Khan
    Sana Khan

Muigizaji mashuhuri wa zamani wa sekta ya filamu ya Bollywood ya India amewajia juu watumiaji wa mitandao ya kijamii wanaomdhihaki na kumkejeli kwa kuvaa vazi la stara la Hijabu.

Sana Khan ambaye mwaka jana aliwashangaza wengi baada ya kutangaza kuachana na kazi ya uigizaji na kukhitari njia ya kiroho na mafundisho ya Uislamu, amewashambulia vikali wanaomkosoa katika mitandao ya kijamii kwa kuvaa mavazi ya kumstiri.

Mfuasi wake mmoja katika mtandao wa kijamii wa Instagram amemuandikia ujumbe wa dhihaka akimuuliza, "kuna maana gani ya kuwa mwanamke mwenye elimu, lakini unajifungia kwenye minyororo ya Hijabu?"

Sana Khan amemjibu kwa kumuambia, "hata ninapokuwa nimevalia Hijabu, naweza kufanya biashara (shughuli) zangu, na niwe na mashemeji na mme mzuri, nini cha ziada ninachokitaka?"

Mcheza filamu huyo wa zamani maarufu wa Bollywood amewahutubu wanaomdhihaki kwa kuvaa Hijabu na kufuata mafundisho sahihi ya Uislamu kwa kuandika: La muhimu zaidi ni kuwa, Allah Ananilinda kwa kila namna, Alhamdulillah. Na pia nimemaliza masomo yangu, je huu si ushindi mkubwa?"

Tangu atangaze kuachana na tasnia ya uigizaji na kufuata Uislamu, nyota huyo wa zamani wa Bollywood amekuwa akituma jumbe za kuhamasisha huku akinukuu aya za Qurani Tukufu katika kurasa zake za mitandao ya kijamii. Ana wafuasi zaidi ya milioni 4 katika mtandao wa kijamii wa Instagram.

Kwa miaka mingi sasa, sekta ya filamu ya Bollywood huko India imekuwa ikiandamwa na kashfa za ubaguzi, ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa kingono na vilevile kashfa za ufuska.