Waislamu Canada wahofishwa na kuongezeka mashambulio ya chuki dhidi yao
Waislamu nchini Canada wamesema kuwa wana wasiwasi na kuongezeka mashambulizi na vitendo vya chuki dhidi yao.
Televisheni ya CBC ya Canada imeripoti kuwa, Waislamu nchini humo wameitaka serikali ya nchi hiyo kuchukua hatua ya kukabiliana na kuzuia vitendo vya chuki, ubaguzi na uhalifu,jinai vinavyotokana na chuki dhidi ya jamii ya Waislamu nchini humo. Waislamu hao wa Canada wamebainisha wasiwasi wao baada ya kujiri hivi karibuni mauaji dhidi ya familia moja ya Kiislamu nchini humo.
Jumapili iliyopita, raia mmoja wa Canada aliyekuwa ndani ya lori aliendesha gari lake na kuwagonga watu wa familia moja ya Waislamu wa nchi hiyo ambao walikuwa wakivuka barara katika mtaa mmmoja wa mji wa London katika jimbo la Ontario nchini humo.
Watu wanne wa familia hiyo ya Kiislamu walipoteza maisha baada ya kugonjwa na raia huyo wa Canada mwenye chuki dhidi ya Waislamu na mtoto wa kiume wa familia hiyo aliyekuwa na miaka 9 kujeruhiwa.
Polisi katika jimbo la Ontario palipojiri mauaji hayo ya chuki dhidi Jumatatu iliyopita ilitangaza kuwa, shambulio hilo lilipangwa mapema; na watu hao waliuliwa kwa sababu tu ni Waislamu.
Kufuatia jinai hiyo ya kutisha, Waislamu nchini Canada huku wakiwa wamepigwa na butwaa na kujawa mshtuko kufuatia mauaji hayo ya kikatili wamelalamikia ukiukiaji wa haki za walio wachache nchini humo na kupuuzwa haki za makundi ya jamii hizo.