"IAEA ipo katika mashinikizo ya Marekani na utawala wa Kizayuni"
Mkuu wa Kamati ya Nishati ya Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) upo chini ya mashinikizo makubwa ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Fereydon Abbasi ambaye pia amewahi kuwa Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomi ya Iran (AEOI) amesema Wamarekani na Wazayuni wanazishinikiza na kuingilia kati utendaji wa IAEA na taasisi nyingine za kimataifa.
Mwansayansi huyo wa nyuklia wa Iran amesema akthari ya wataalamu wa IAEA ni Wamarekani na Wazayuni, na wamekuwa wakivujisha taarifa za ukaguzi wao kwa tawala za kibeberu. Abbasi amesisitiza kuwa, "matokeo ya kaguzi za IAEA yanaweza kupatikana kiwepesi na wataalamu wa Maghaibi."
Mkuu wa Kamati ya Nishati ya Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu ya Iran ameeleza bayana kuwa, "Jamhuri ya Kiislamu ipo chini ya mashinikizo mengi na vikwazo mbalimbali, kwa msingi huo IAEA inapaswa kulinda barabara data za Iran."
Siku ya Jumatano, Msemaji wa Taasisi ya Atomiki ya Iran (AEOI), Behrouz Kamalvandi alikosoa hatua ya Wakala wa KImataifa ya Nishati ya Atomiki kutoa taarifa za siri za Iran na kuwapa washirika wengine na kusisitiza kuwa, mwenendo huo unapaswa kukomeshwa haraka iwezekanavyo.
Iran imekuwa ikisisitiza kuwa, wakala wa IAEA unapaswa kujiepusha na masula ya siasa katika utendaji wake kwa ajili kulinda uhuru wake, na vile vile kutoegemea upande wowote.