HRW yakosoa marufuku ya vazi la hijabu nchini India
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetangaza kuwa marufuku ya vazi la hijab inakiuka wajibu wa India chini ya sheria ya kimataifa ya haki za binadamu, ambayo inadhamini haki ya uhuru wa imani ya kidini ya mtu binafsi na uhuru wa kujieleza na kupata elimu bila ubaguzi.
Marufuku ya kuvaa hijabu iliyowekwa katika vyuo vya jimbo la Karnataka imeamsha wimbi la hasira za wanafunzi Waislamu, ambao wanasema, hiyo ni hujuma inayolenga imani yao ambayo inatambuliwa rasmi na katiba ya India, huku makundi ya Kihindu ya mrengo wa kulia yakitumia mabavu kuwazuia mabanati wa Kiislamu wasiingie vyuoni na hivyo kuibua mivutano ya kijamii jimboni humo.
Kupamba moto mzozo juu ya vazi la hijabu katika vyuo hivyo kumetumiwa vibaya na maafisa wa serikali ya India ambao sasa wamepiga marufuku vazi hilo na vilevile skafu za rangi ya zafarani za Wahindu wafuasi wa chama tawala cha BJP.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesisitiza kuwa, kupiga marufuku vazi la hijabu ni mojawapo ya mifano ya hivi karibuni ya juhudi za mamlaka ya India kuwatenga Waislamu na kuzidisha ukatili dhidi yao.
Tarehe 7 mwezi huu wa Februari mamia ya wanafunzi waliokuwa wakiandamana na wazazi wao walifanya maandamano wakidai haki yao ya kuhudhuria mashuleni wakiwa na vazi ya hijabu.
Ijumaa ya jana pia maelfu ya wanawake nchini India na Pakistan walifanya maandamano makubwa kupinga marufuku ya vazi la hijabu mashuleni katika jimbo la Karnataka nchini India.
Marufuku ya kuvaa hijabu iliyowekwa katika vyuo vya jimbo la Karnataka imeamsha wimbi la hasira za wanafunzi Waislamu, ambao wanasema, hiyo ni hujuma inayolenga imani yao ambayo inatambuliwa rasmi na katiba ya India, huku makundi ya Kihindu ya mrengo wa kulia yakitumia mabavu kuwazuia mabanati wa Kiisalmu wasiingie vyuoni na hivyo kuibua mivutano ya kijamii jimboni humo.
Takriban watu milioni 200 katika jamii yenye watu bilioni 1.4 wa India ni Waislamu.