Mwito wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa Taliban
https://parstoday.ir/sw/news/world-i81816-mwito_wa_baraza_la_usalama_la_umoja_wa_mataifa_kwa_taliban
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeitaka Taliban ichukue hatua haraka iwezekanavyo kuhakikisha wasichana nchini Afghanistan wanarudi mashuleni kuendelea na masomo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 27, 2022 02:30 UTC
  • Mwito wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa Taliban

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeitaka Taliban ichukue hatua haraka iwezekanavyo kuhakikisha wasichana nchini Afghanistan wanarudi mashuleni kuendelea na masomo.

Baraza la Usalama limesisitiza katika taarifa maalumu liliyotoa kwamba, uamuzi wa Taliban wa kuendelea kuzifunga skuli za wasichana unakinzana na ahadi yake ya kuwa na maelewano chanya na jamii ya kimataifa.

Kikao cha Baraza la Usalama la UN

Baada ya kundi la Taliban kushika tena hatamu za utawala nchini Afghanistan Agosti 15, 2021, si tu lilifuta aina nyingi za ajira na njia za kupatia riziki, lakini pia liliwapiga marufuku wasichana na watoto wa kike kwenda vyuo vikuu na mashuleni. Licha ya ahadi ilizotoa Taliban za kujenga maelewano na jamii ya kimataifa kwa kuunda serikali inayowajibika na inayoheshimu haki za raia wake, lakini ukweli ni kuwa, hadi sasa kundi hilo halijatekeleza hata moja kati ya ahadi hizo. Baadhi ya duru zinasema, kuzuiliwa skuli za wasichana zisifunguliwe tena nchini Afghanistan licha ya ahadi iliyokuwa imetoa Taliban, kumezusha tofauti na mivutano baina ya viongozi waandamizi wa kundi hilo na kufanyika mabadiliko ndani ya serikali yake. Hata hivyo inavyoonekana, kupinga ushiriki wa wanawake na wasichana katika masuala ya kijamii likiwemo la elimu ni sera rasmi, mstari mwekundu na moja ya masuala ya kiitikadi  ya Taliban, kiasi kwamba ni vigumu kuamini kama kundi hilo litaweza kulifumbia macho.

Lakini ajabu ni kuwa, uchunguzi uliofanywa na baadhi ya mitandao na chaneli za habari za Afghanistan, ukiwemo "mtandao wa wachambuzi" unaonyesha kuwa, watoto wa baadhi ya viongozi wa Taliban, hususan mabanati wao wanaendelea na masomo katika nchi za nje ikiwemo Qatar. Kwa mujibu wa mjumbe mmoja wa wawakilishi wa Taliban katika mazungumzo na Marekani, watoto wa kike wa mawaziri wa serikali ya Taiban wanasomea kozi mbalimbali ikiwemo ya utabibu katika vyuo vikuu vya Qatar na skuli za Wapakistan zilizoko nchini humo.

Watoto wa kiume wakiwa darasani wakati baadhi ya skuli za wasichana zimefungwa Afghanistan

Hii inamaanisha kuwa, upinzani wa Taliban kwa suala la wasichana kuendelea na masomo nchini Afghanistan ni pambo tu la kile kinachotajwa kama sera za kidini za kundi hilo, zinazotumiwa kuvutia na kutaka kuungwa mkono sera na siasa zake na tabaka la jamii ya Waafghani wenye mitazamo ya jadi. Kwa sababu, kitendo cha viongozi wa Taliban cha kuwaandikisha mabinti zao katika vyuo vikuu na skuli za Wapakistani na za Qatar kinadhihirisha sera ya undumakuwili wanayoitumia viongozi hao kuhusiana na watu wa Afghanistan, jambo ambalo kadiri litavyozidi kufichuliwa litaharibu sura ya Taliban mbele ya Waafghani, hasa wa familia za jadi zinazoheshimu na kutukuza itikadi za kundi hilo.

Wakati huohuo, ripoti iliyotolewa na gazeti la Daily Telegraph linalochapishwa nchini Uingereza inaeleza kuwa, katika mahojiano liliyofanya gazeti hilo na baadhi ya viongozi na mawaziri wa serikali ya Taliban, kila mmoja kati ya viongozi hao amesema, anataka kuongeza mke wa pili ambaye ni msomi. Na sababu yake ni kwamba, kufanya hivyo kutawafanya watoto wake wapate malezi mazuri. Si hayo tu, viongozi wa Taliban wamewapeleka mabinti zao skuli za nje ya Afghanistan zinazosomesha kwa lugha ya kigeni na kutoa mafunzo ya kompyuta na hivi sasa wanaendelea kimyakimya na masomo yao huko.

Viongozi wa Taliban

Alaa kulli hal, huku Taliban ikijionyesha kuwaonea uchungu wananchi na kuheshimu haki za binadamu za raia wa Afghanistan, kila mara inadai kuwa imeshatimiza masharti yote yanayotakiwa ili serikali yake itambuliwe kimataifa. Lakini kwa upande wa matendo, si tu haijatimiza ahadi zake za kutekeleza hata haki ya kawaida kabisa ya watu wa Afghanistan, ambayo ni kuwapatia elimu, bali kutokana na kuhalifu ahadi ilizotoa, inaandaa mazingira ya uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo. Isitoshe, hatua hiyo inaweza kuharibu zaidi sura ya Taliban katika duru za kikanda na kimataifa na kupelekea kusitishwa misaada yoyote ile ya kibinadamu kwa wananchi wa Afghanistan ili kulalamikia utendaji mbovu wa Taliban; jambo ambalo kama litatokea, ni wananchi hao ndio watakaokuwa mhanga wa sera mbovu na za kiundumakuwili za viongozi wa kundi hilo.../