Russia: Marekani imekiuka mkataba wa silaha za kibaolojia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i82144-russia_marekani_imekiuka_mkataba_wa_silaha_za_kibaolojia
Naibu mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa, Dmitry Polyansky, ameuambia mkutano wa waandishi wa habari mjini New York kwamba shughuli za kijeshi za kibaolojia za Marekani nchini Ukraine zinakiuka Mkataba wa Silaha za Kibaolojia.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Apr 04, 2022 21:51 UTC
  • Russia: Marekani imekiuka mkataba wa silaha za kibaolojia

Naibu mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa, Dmitry Polyansky, ameuambia mkutano wa waandishi wa habari mjini New York kwamba shughuli za kijeshi za kibaolojia za Marekani nchini Ukraine zinakiuka Mkataba wa Silaha za Kibaolojia.

Akitoa taarifa yake kuhusu nyaraka zilizogunduliwa na Wizara ya Ulinzi ya Russia kuhusiana na shughuli za kibaolojia za kijeshi za Marekani nchini Ukraine, Dmitry Polyansky amesema: "Tunachambua ushahidi unaoonesha kuhusika moja kwa moja mamlaka ya kisiasa ya Marekani katika kufadhili shughuli za kijeshi za kibaolojia nchini Ukraine."

Polyansky pia amesema kuwa Wizara ya Ulinzi ya Russia imepata ushahidi kwamba maafisa wa Ukraine, chini ya usaidizi wa moja kwa moja na mwongozo wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani, walikuwa wakitekeleza miradi na majaribio hatari kama sehemu ya mpango wa kibaolojia wa kijeshi. Shughuli hizo zimekuwa zikifanyika kwa miaka mingi kwenye ardhi ya Ukraine katikati mwa Ulaya Mashariki na katika umbali wa karibu kabisa na mipaka ya Russia, na zimekuwa tishio kubwa kwa usalama wa kibiolojia wa Russia na eneo hilo kwa ujumla.

Dmitry Polyansky

Kashfa hiyo mpya ya hatua za Marekani katika kuisaidia Ukraine kuunda silaha za kibaolojia, inaonyesha hali halisi na isiyo ya kibinadamu na nia ya Washington ya kutengeneza aina mbalimbali za vimelea vya kibaolojia nchini Ukraine chini ya madai ya ushirikiano wa kiulinzi baina ya nchi hizo mbili. Pamoja na hayo Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imedai kuwa Washington haina maabara nchini Ukraine. Hata hivyo ushahidi unaonyesha kuwa, Pentagon inasimamia moja kwa moja maabara hizo na kwamba wakandarasi wake wanaongoza miradi inayohusiana na shughuli hizo.

Nikolai Patrushev, Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia amesema: “Ulimwengu uliostaarabika hatimaye utaona kwamba Marekani inaendeleza sera za Ujerumani ya Wanazi na utawala wa Hitler na kufanya majaribio yasiyo ya kibinadamu kwa kutumia wanadamu.”

Hatua ya Marekani ya kukana uwepo wa maabara za kutengeneza silaha za kibaolojia nchini Ukraine imechukuliwa wakati nyaraka na ushahidi unaonyesha kwamba, Washington ililipa kipaumbele maalumu suala la kuanzisha maabara za silaha za kibaolojia katika nchi za Urusi ya zamani. Ingawa Marekani imetia saini Mkataba wa Silaha za Kibaolojia ambao uliidhinishwa mwaka wa 1972 na kuanza kutumika 1975, lakini kwa hakika inaongoza katika kustawisha aina mbalimbali za silaha hizo hatari kwa binadamu. Zaidi ni kwamba, eneo zilikojengwa maabara hizo, haswa zile zilizo katika nchi jirani na Russia na China, zinalenga kuanzisha vitisho la kibaolojia dhidi ya washindani hao wawili wakuu wa kimataifa wa Marekani. 

Kuwepo kwa maabara za kibaolojia za Marekani katika maeneo mbalimbali ya duniani kunaonyesha jinsi Washington inavyopuuza maisha ya binadamu duniani, na vilevile sera za nchi hiyo za kuendelea kutengeneza silaha za maangamizi ya umati. Ukweli ni kwamba, hatua ya Washington ya kukanusha kuhusika ya maabara za silaha za kibaolojia nchini Ukraine licha ya kuwepo nyaraka na ushahidi usio na shaka, inaonesha kwamba, maofisa wa Marekani wanafahamu vyema uharibifu na hatari kubwa ya shughuli hizo katika vituo na maabara zake; kwa sababu hiyo wanapinga uhusiano wa aina yoyote wa Pentagon na maabara hizo.  

Mbali na kuwa na makumi ya maabara kubwa za kibaolojia ndani ya nchi, katika miaka ya hivi karibuni Marekani pia imelipa kipaumbele maalumu suala la kujenga maabara za silaha za kibaolojia nje ya nchi hiyo, na inakadiriwa kuwa Washington ina maabara zaidi ya 200 za kibaolojia katika maeneo mbaliimbali ya duniani. Washington imehamishia maabara zake nyingi nje ya Marekani ili kuzuia majanga ya kibaolojia kama yale yaliyowahi kutokea nchi humo katika miaka ya huko nyuma.