Kuongezeka malalamiko ya kimataifa dhidi ya Israel
Taasisi 16 za kimataifa kote ulimwenguni zimeandika barua zikilaani kitendo cha utawala wa Kizayuni wa Israel cha kumpiga marufuku ya kusafiri, Omar Barghouthi, mwasisi wa Harakati ya Kimataifa ya Kuisusia Israel BDS.
Taasisi hizo za kimataifa kutoka katika nchi za bara la Amerika, Asia na Ulaya aidha zimetaka kupunguzwe ukatili na jinai dhidi ya viongozi na jumuiya za kiraia za Palestina. Omar Barghouthi, mwasisi wa Harakati ya Kimataifa ya Kuisusia Israel, ni Mpalestina aliyezaliwa nchini Qatar na hivi sasa anaishi katika mji wa Acre wa kaskazini mwa ardhi za Palestina zinayokaliwa kwa mabavu. Hivi sasa utawala wa Kizayuni umempiga marufuku ya kutembea ndani na nje ya mji huo na kila anapotaka kwenda kwenye eneo jingine, analazimika aombe kibali maalumu kutoka kwa mamlaka za Kizayuni. Barghouthi alianzisha Harakati ya Kimataifa ya Kuisusia Israel mwaka 2005, na lengo la harakati hiyo ni kuushinikiza utawala wa Kizayuni uache kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina na iheshimu haki ya Wapalestina ya kurejea katika ardhi zao kwa mujibu wa azimio nambari 194 la Umoja wa Mataifa. Matukio ya kimataifa yanaonesha kukasirishwa mno walimwengu na utawala wa Kizayuni kama ambavyo yanaonesha nafasi ya Harakati ya Kimataifa ya Kuisusia Israel katika fikra za walio wengi ulimwenguni, kiasi kwamba waungaji mkono wa harakati hiyo wako hadi katika nchi ambazo ni waungaji mkono wakuu wa utawala wa Kizayuni, yaani Marekani na Uingereza. Uchunguzi wa maoni uliofanyika nchini Marekani na kutangazwa na Kanali ya Pili ya televisheni ya utawala wa Kizayuni wa Israel unaonesha kuwa, idadi ya kutosha ya raia wa Marekani na Uingereza wanaamini kuwa, kuna kila sababu ya kuwekewa vikwazo Israel kutokana na jinai zake. Kadiri siku zinavyopita ndivyo walimwengu wanavyozidi kuiona sura ya kikatili, fasidi na ya kibaguzi ya utawala wa Kizayuni. Aidha kutokana na mashinikizo ya wananchi, hata tawala za nchi za Ulaya ambazo daima zimekuwa zikiuunga mkono utawala wa Kizayuni, sasa zinalazimika kulalamikia ukaidi wa viongozi wa utawala wa Kizayuni wa kutojali maazimio ya kimataifa. Ukosoaji mkali wa nchi za Ulaya katika miezi ya hivi karibuni dhidi ya kuongezeka vitendo vya ukandamizaji na kujitanua vya Israel ni uthibitisho wa kumalizika uungaji mkono wa pande zote wa nchi za Ulaya kwa utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na mashinikizo ya wananchi. Wakati huo huo, Harakati ya Kimataifa ya Kuisusia Israel BDS inaungwa mkono na jumuiya mbalimbali za kijamii, makundi ya kidini, taasisi zisizo za kiserikali na tawala za wananchi katika kona mbalimbali za dunia, na kila leo uungaji mkono huo unazidi kuongezeka. Vikwazo vilivyowekwa dhidi ya utawala wa Kizayuni na madhara ya vikwazo hivyo katika nyuga za kisiasa, kidiplomasia, kiutamaduni na kiuchumi, vimekuwa na madhara makubwa kwa utawala pandikizi wa Kizayuni. Tena hayo ni kwa mujibu wa utafiti wa usalama wa taifa uliofanywa na utawala wa Kizayuni wenyewe ambapo utafiti huo unaonesha kuwa, Israel imepata hasara ya dola bilioni 31 kutokana na vikwazo vya kimataifa katika miaka ya hivi karibuni. Weledi wa masuala ya Israel wanaamini kuwa, hasara za kiuchumi ilizopata utawala wa Kizayuni na vitongoji vya walowezi wa Kizayuni ni zaidi ya dola bilioni nane kwa mwaka. Kiujumla ni kuwa, sisitizo la kimataifa la kulindwa haki za wananchi wa Palestina na kuwekewa vikwazo utawala wa Kizayuni ni ishara kuwa dunia imechoshwa na jinai za Israel na kwamba anga ya kimataifa inaendelea kubadilika kwa faida ya Wapalestina na kwa madhara ya utawala wa Kizayuni wa Israel.