Jamhromi: Ufaransa ilihusika moja kwa moja katika mauaji ya kimbari Rwanda
https://parstoday.ir/sw/news/world-i82262-jamhromi_ufaransa_ilihusika_moja_kwa_moja_katika_mauaji_ya_kimbari_rwanda
Msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Ufaransa ilihusika moja kwa moja katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Apr 07, 2022 22:57 UTC
  • Jamhromi: Ufaransa ilihusika moja kwa moja katika mauaji ya kimbari Rwanda

Msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Ufaransa ilihusika moja kwa moja katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda.

Ali Bahadori Jahromi amesema hayo kwa mnasaba wa kuwadia mwaka wa 28 tangu yatokee mauaji hayo ya kimbari yaliyoishtua dunia na kuongeza kuwa: Nchi za Magharibi kama Ufaransa zilihusika moja kwa moja kwenye mauaji ya kimbari ya Rwanda kwa kutuma silaha nchini humo.

Msemaji wa serikali ya Iran amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, ambao ameuambatanisha na ripoti ya shirika la habari la Reuters yenye kichwa kisemacho: Emmanuel Macron akiri Ufaransa ilihusika katika mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994.

Jahromi ameongeza kuwa: Yalikuwa mauaji ya kimbari ya wazi ambayo kila mmoja aliyaona na kuyanyamazia kimya, na baadhi ya nchi za Magharibi kama Ufaransa zilikuwa na nafasi kubwa kwenye mauaji hayo.

Ali Bahadori Jahromi

Ikumbukwe kuwa, Aprili 6 mwaka 1994, yalianza mauaji makubwa yalifanywa na utawala wa wakati huo wa Rwanda uliokuwa ukiongozwa na kabila la Wahutu dhidi ya wenzao wa kabila la Tutsi.

Katika mauaji hayo Wahutu wenye misimamo mikali waliwauwa raia wa Kitutsi na Wahutu wenye misimamo ya wastani karibu milioni moja na kuwafanya wengine zaidi ya milioni mbili kuwa wakimbizi. 

Uchunguzi maalumu uliofanywa mwaka 2016 ulifichua kuwa, maafisa 22 wa jeshi la Ufaransa walihusika moja kwa moja katika mauaji hayo ya kimbari ya nchini Rwanda.