Russia yawawekea vikwazo Makamu wa Rais wa Marekani, Mkuu wa Meta
Serikali ya Russia imetangaza kuwawekea vikwazo makumi ya shakhsia wa Marekani akiwemo Makamu wa Rais wa nchi hiyo, Kamala Harris na Afisa Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya Meta (Facebook) Mark Zuckerberg.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imesema shakhsia 29 wa Marekani wakiwemo wafanyabiashara wakubwa, wataalamu na waandishi wa habari wanaoendesha kampeni kubwa ya propaganda dhidi ya Moscow wamejumuishwa kwenye orodha hiyo mpya ya vikwazo, ikiwa ni jibu kwa wimbi la vikwazo la utawala wa Joe Biden dhidi ya Warusi.
Aidha raia 61 wa Canada wakiwemo maafisa wa ngazi za juu wa serikali ya nchi hiyo, wakuu wa Wizara ya Ulinzi na wanahabari wamo kwenye vikwazo hivyo vipya vya Moscow, na hawatoruhusiwa kutia mguu nchini Russia.
Kufuatia operesheni ya kijeshi ya Russia dhidi ya Ukraine iliyoanza Februari 24 , kambi ya Magharibi ikiongozwa na Marekani imeiwekea Moscow vikwazo vikali vya kiuchumi, ambavyo hata hivyo vimekuwa na taathira hasi pia kwa chumi za Wamagharibi wenyewe.
Haya yanajiri siku chache baada ya gazeti la Washington Post kuripoti kuwa, vikwazo vya Washington dhidi ya Russia vimekuwa chachu ya kushadidisha mfumko wa bei za bidhaa unaoshuhudiwa hivi sasa nchini Marekani.
Aidha Shirika la Fedha Duniani (IMF) lilionya hivi karibuni kuwa, vikwazo dhidi ya Russia huenda vikadhoofisha na kuipotezea umashuhuri sarafu ya dola ya Kimarekani.