Taliban yatoa wito kwa Waislamu duniani kusimama dhidi ya Israel
https://parstoday.ir/sw/news/world-i82944-taliban_yatoa_wito_kwa_waislamu_duniani_kusimama_dhidi_ya_israel
Naibu msemaji wa serikali ya mpito ya Taliban nchini Afghanistan amesema umoja ni msingi wa Uislamu na hivyo kadhia ya Palestina inapaswa kushughulikiwa kwa msingi huo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 26, 2022 11:08 UTC
  • Taliban yatoa wito kwa Waislamu duniani kusimama dhidi ya Israel

Naibu msemaji wa serikali ya mpito ya Taliban nchini Afghanistan amesema umoja ni msingi wa Uislamu na hivyo kadhia ya Palestina inapaswa kushughulikiwa kwa msingi huo.

Akizungumza kwa mnasaba wa kukaribia Siku ya Kimataifa ya Quds, Ana'mollah Samangani amesema kwa kuzingatia msingi wa umoja wa Umma wa Kiislamu, Waislamu wote wanapaswa kuungana katika kuangamiza udhalimu wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wa Palestina.

Akizihutubu tawala za Kiarabu ambazo zimeanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel, Samangani amezitahadharisha kuhusu kufikia mapatano yoyote na utawala huo ulio dhidi ya Waislamu.

Aidha ametoa wito kwa Waislamu duniani kutosahau kadhia ya Palestina, matatizo ya Wapalestina na Msikiti wa al Aqsa ambao ni qibla cha kwanza cha Waislamu.

Enamullah Samangani

Ikumbukwe kuwa Ijumaa 15 Aprili wanajeshi wa utawala wa Kizayuni walitekeleza hujuma dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa ambapo waliwashambulia waumini waliokuwa wakitekeleza ibada katika msikiti huo katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani. Katika hujuma hiyo, zaidi ya waumini 160 walijeruhiwa na wengine 400 walikamatwa na askari hao vamizi wa Israel. Uchokozi huo umelaaniwa vikali kimataifa na pia katika nchi za Kiislamu na Kiarabu. Hujuma hiyo ambayo inaendelea kulaaniwa kimataifa imekuja huku baadhi ya nchi za Kiarabu zikiwa zimeanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni ambao unazikoloni ardhi za Palestina.

Hivi karibuni nchi nne za Kiarabu ambazo ni, Bahrain, Misri, Moroco na UAE, zilishiriki katika kikao kilichohudhuriwa na Marekani na Israel katika eneo la Negev linalokaliwa kwa mabavu na Israel.