Russia yawafukuza wanadiplomasia 7 wa Denmark kulipiza kisasi
Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imetoa taarifa na kutangaza kuwa, nchi hiyo inawatambua wanadiplomasia saba wa ubalozi wa Denmark huko Moscow kuwa watu wasiofaa na imechukua uamuzi wa kuwafukuza nchini humo.
Sergey Lavrov amesema hayo na kusisitiza katika taarifa yake kuwa: Balozi wa Denmark huko Moscow ameelezwa kwamba Russia inawahesabu wanadiplomasia hao saba wa Denmark kuwa watu wasiofaa na imewafukuza nchini humo; kama moja ya hatua zake za kulipiza kisasi hatua zilizochukuliwa na Denmark na nchi za Magharibi dhidi yake.
Russia imesema kuwa wanadiplomasia hao 7 wa Denmark wanapewa muda wa wiki mbili wahakikishe wameshaondoka nchini humo. Katika upande mwingine, Russia pia imemnyima viza ya kuingia nchini humo mwanadiplomasia mmoja wa Denmark kama sehemu ya kulipiza kisasi hatua zilizochukulwa dhidi yake na nchi za Magharibi.
Awali ilitangazwa kuwa, Denmark imewafukuza wanadiplomasia 15 wa Russia kwa kisingizio cha kuwepo changamoto za kiusalama. Wakati huo huo Russia ilijibu hatua hiyo ya Copenhagen dhidi yake ikisisitiza kuwa, Moscow italipiza kisasi hatua hiyo ya Denmark.
Aidha Denmark siku kadhaa zilizopita ilimuita kumuhoji Balozi wa Russia nchini humo kwa kisingizio kwamba ndege ya Russia ilikiuka anga ya Denmark. Vita vya kidiplomasia vinazidi kupamba moto kati ya nchi za Magharibi na Moscow kufuatia vita vilivyoanzishwa na Russia huko Ukraine.