Kushindwa Umoja wa Ulaya kuiwekea vikwazo vya mafuta Russia
(last modified Wed, 18 May 2022 03:04:07 GMT )
May 18, 2022 03:04 UTC
  • Kushindwa Umoja wa Ulaya kuiwekea vikwazo vya mafuta Russia

Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema katika mkutano wake na waandishi wa habari baada ya kikao cha mawaziri wa umoja huo mjini Brussels Ubelgiji kwamba, hakuna uwezekano wa kufikiwa makubaliano kuhusiana na kifurushi cha sita cha vikwazo dhidi ya Russia.

Borrell amesema: Hatuna kauli moja kuhusiana na vikwazo vya mafuta vya Russia. Aidha mwanadiplomasia huyo wa Ulaya amekiri kwamba, viongozi wa Umoja wa Ulaya hawawezi kufikia makubaliano ya kuiwekea Russia vikwazo vya mafuta.

Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi 27 za Ulaya Jumatatu ya juzi walikutana na kujadili kuhusiana na kifurushi cha sita cha vikwazo dhidi ya Russia ambacho kinajumuisha kusimamisha uingizaji wa mafuta barani humo kutoka Russia. Hata hivyo mawaziri hao walishindwa kufikia mwafaka, kutokana na upinzani mkali wa Hungary ambayo inadhamini 65% ya nishati yake ya mafuta kutoka Russia. Ili Umoja wa Ulaya uweze kupasisha vikwazo hivyo, unahitajia kura za ndio za nchi 27 za umoja huo.

Kamisheni ya Umoja wa Ulaya ilipendekeza kwamba, uingizaji wa mafuta ya Russia barani humo usitishwe kwa muda wa miezi sita na uingizaji wa bidhaa za Russia zinazotokana na mafuta nao ukomeshwe hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu. Aidha kwa mujibu wa mapendekezo hayo, Sberbank ambayo ni benki kubwa zaidi ya Russia iondolewe katika mfumo wa kimataifa wa mabadilishano ya kifedha baina ya benki ujulikanao kama SWIFT.

 

Pamoja na hayo nchi ya Hungary ni mpinzani mkuu wa vikwazo hivyo dhidi ya Russia. Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya ameashiria msimamo huo wa Budapest na kusema kuwa, mazungumzo ya juzi yameweka wazi baadhi ya matatizo ambayo Hungary inakabiliwa nayo.

Péter Szijjártó, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Hungary alisema Jumatano iliyopita kwamba, nchi hiyo itavipigia kura ya  ndio vikwazo vya mafuta dhidi ya Russia pale tu umoja huo utapakuja na njia mbadala ya utatuzi wa matatizo yatayojitokeza baada ya hatua hiyo. Aidha amesema nchi yake haikubaliani na suala la kuongezwa mno bei ya mafuta na kupatikana mafuta mbadala ya Russia ni jambo ambalo haliwezekani isipokuwa kwa himaya na uungaji mkono wa kifedha wa Umoja wa Ulaya.

Ukweli wa mambo ni kuwa, Hungary inahesabiwa kuwa mmoja wa washirika wa karibu wa Russia katika Umoja wa Ulaya na ikiwa na lengo la kupunguza gharama zinazotokana na vikwazo vya mafuta ghafi ya Russia imeomba kupatiwa na umoja huo mamia ya mamilioni ya Euro.

Kwa muktadha huo, imefahamika wazi sasa kwamba, hakuna msimamo mmoja barani Ulaya kuhusiana na suala la kuiwekea vikwazo vya mafuta Russia. Ukweli wa mambo ni kuwa, kundi la nchi ambazo zina utegemezi kwa mafuta ya Russia siyo jambo jepesi kwao kuweka kando hilo na kisha kutafuta chaguo jingine. Jambo hilo haliwezekani kufanyika hususan katika kipindi cha muda mfupi na hilo linaweza kuwa na hasara kubwa kwa uchumi wao.

Rais Putin wa Russia ametia saini amri ya kuiwekea vikwazo vya ulipizaji kisasi kambi ya Magharibi

 

Richard Sulik, Waziri wa Uchumi wa Slovakia alionya hivi karbuni kuhusiana na kuwekewa vikwazo vya mafuta nchi ya Russia. Waziri Richard alisema: Kupiga marufuku uingizaji wa mafuta ya Russia barani Ulaya, kutasambaratishha kabisa uchumi wa bara hilo sambamba na kuziathiri pakubwa nchi za Slovakia, Austria, Jamhuri ya Czech na Ukraine.

Mkabala na nchi hizo, kuna kundi la mataifa ambayo ni waitifaki wa Marekani ambayo yamekuwa yakishinikiza Russia iwekewe vikwazo vya mafuta. Baadhi ya mataifa hayo ni Uingereza, Poland na mataifa ya Ukanda wa Baltic. Mintarafu hiyo inaonekana kuwa, filihali Ulaya ipo katika njia panda mbili. Njia ya kwanza ni kuchagua maslahi yao ya kiuchumi na hivyo kuendelea kuingiza mafuta na gesi barani humo kutokea Russia na kwa msingi huo kustawisha uchumi na kuzuia kujitokeza hasara kubwa kwa mataifa hayo. Chaguo la pili ni kuungana na Marekani katika fremu ya malengo makubwa ya kijiopolitiki ya Magharibi yaani kukabiliana na nguvu za kimataifa ambazo zinataka kuweko mabadiliko katika nidhamu ya sasa ya duunia hususan Russia na katika hatua ya pili China. Christian Lindner, Waziri wa Fedha ya Ujerumani anasema: Vita vya Ukraine na Russia vitapelekea kutokea mfumo mpya katika dunia.

Vita vya Ukraine

 

Yote haya yanaonyesha wazi mtazamo unaotawala baina ya mataifa ya Ulaya. Filihali, Umoja wa Ulaya upo katika kambi ya kuiunga mkono Ukraine na madola hayo yamejiunga katika safu ya kuiwekea vikwazo Russia na hivyo kuamua kuwa pamoja na Marekani na malengo ya kijiopolitiki ya Magharibi.

Pamoja na hayo, upinzani wa mataifa kama Slovakia na Hungary kwa uamuzi wa Umoja wa Ulaya kuhusiana na suala la kuiwekea vikwazo vya mafuta Russia ni jambo linaloonyesha wazi kuwa, ndani ya Ulaya hakuna msimamo na mtazamo mmoja kuhusiana na hatua hiyo; kwani baadhi ya mataifa ya bara hilo hayako tayari kuyatoa muhanga maslahi yao ya kitaifa kwa ajili ya maslahi na malengo makubwa ya Marekani.

Fauka ya hayo ni kuwa, kwa mtazamo wa mataifa hayo kushadidisha mzozo na mvutano na Russia katika uga wa kiuchumi, nishati, usalama na kijeshi ni jambo lenye hatari kubwa kwa usalama wa Ulaya.

Tags