Taliban: Mashinikizo dhidi ya Afghanistan hayana tija yoyote
https://parstoday.ir/sw/news/world-i84116-taliban_mashinikizo_dhidi_ya_afghanistan_hayana_tija_yoyote
Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Taliban iliyoko mjini Doha, Qatar amekaribisha vikao vilivyoitishwa kuzungumzia hali ya Afghanistan na kusisitiza kuwa siasa za mashinikizo dhidi ya nchi hiyo haziwezi katu kuwa na tija na kwamba dunia inapaswa kujenga maelewano na Afghanistan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 28, 2022 03:43 UTC
  • Taliban: Mashinikizo dhidi ya Afghanistan hayana tija yoyote

Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Taliban iliyoko mjini Doha, Qatar amekaribisha vikao vilivyoitishwa kuzungumzia hali ya Afghanistan na kusisitiza kuwa siasa za mashinikizo dhidi ya nchi hiyo haziwezi katu kuwa na tija na kwamba dunia inapaswa kujenga maelewano na Afghanistan.

Licha ya kupita miezi tisa tangu Taliban iliposhika hatamu za madaraka nchini Afghanistan, kutokana na baadhi ya sera zinazotekelezwa na kundi hilo ikiwemo ya mbinyo dhidi ya wanawake, jamii ya kimataifa bado haijaitambua serikali ya muda ya Taliban.

Suhail Shaheen, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya serikali ya muda ya Taliban, iliyoko nchini Qatar amezungumzia mkutano wa siku mbili wa nchi za ukanda huu unaofanyika nchini Tajikistan kwa lengo la kujadili kadhia ya Afghanistan na kusisitiza kuwa, mamlaka za utawala za Afghanistan hazitaruhusu ardhi ya nchi hiyo itumike dhidi ya nchi zingine.

Huku akieleza kwamba mashinikizo dhidi ya serikali ya Taliban hayana faida yoyote, Shaheen amesisitiza kuwa mbinu za mashinikizo haziwezi kuwa na tija nchini Afghanistan.

Viongozi wa Taliban

Ametilia mkazo msimamo wa Taliban wa kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na nchi za eneo na kuongezea kwa kusema: kama mtu ana jambo lolote lile, sisi tuko tayari kulitatua kupitia njia ya amani.

Katika mkutano wa Tajikistan washauri wa usalama wa taifa wa Tajikistan, India, Russia, Kazakhstan, Uzbekistan, Iran, Kirgizistan na China wanajadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu hali ya Afghansitan na eneo kwa jumla.../