Tetemeko la ardhi Afghanistan laua karibu watu elfu moja, uokoaji unaendelea
Ripoti za mashirika ya habafri zinasema kuwa karibu watu 1,000 wameaga dunia na mamia kujeruhiwa katika tetemeko la ardhi lililoikumba mikoa miwili kusini mashariki mwa Afghanistan leo, Jumatano.
Mapema leo, Shirika la Kudhibiti Majanga la Afghanistan lilitangaza kuwa tetemeko la ardhi lililotokea mashariki mwa nchi hiyo limesababisha vifo vya mamia ya watu na kujeruhiwa wengine wengi.
Shirika la Habari la Reuters limeripoti kuwa Waafghani wasiopuungua 950 wamefariki dunia na mamia ya wengine wamejeruhiwa katika tetemeko hilo lililokuwa na nguvu ya dajara 6.1 kwa kipimo cha Rishta.
Mkuu wa Shirika la Kudhibiti Majanga la Afghanistan, Mohammad Nassim Haqqani amesema idadi kubwa ya vifo vilivyothibitishwa vimetokea katika mkoa wa Paktika.
Msaidizi wa msemaji wa serikali ya Afghanistan, Bilal Karimi amesema nyumba nyingi za maeneo yaliyokumbwa na tetemeko hilo zimeharibiwa, na wakazi wake bado wako chini ya vifusi. Ripoti zinasema, kuna uwezekano wa idadi ya vifo kuongezeka.
Idara ya Jiolojia ya Marekani imeripoti mapema leo kuwa, zilzala hiyo iliyokuwa na ukubwa wa 6.1 kwa kipimo cha rishta ilipiga eneo la kilomita 44 kutoka mji wa Khost karibu na mpaka wa Pakistan na katika kina cha kiomita 51.
Hedayatullah Paktin ambaye ni mwanahabari na mwandishi wa masuala ya kisiasa amesema, akthari ya nyumba katika mkoa wa Paktika hujengwa kijadi kwa kutumia udongo, mawe na vifaa vingine na kwamba ni nadra kushuhudia nyumba zilizojengwa kwa kutumia zege.
Kwa mujibu wa kituo cha Jiolojia cha Ulaya na Mediterania (EMSC), mtikisiko wa tetemeko hilo umehisika na watu wapatao milioni 119 katika nchi za Pakistan, Afghanistan na India na katika eneo lenye ukubwa wa kilomita 500.