Vifo vya wazee kwa kutumia mihadarati vyaongezeka Marekani
Ripoti mpya ya utafiti inaonesha kuwa, idadi ya wazee wenye umri wa miaka 65 na zaidi wanaopoteza maisha kutokana na matumizi ya mihadarati nchini Marekani imeongezeka sana.
Utafiti uliofanywa na Kituo cha Kitaifa cha Takwimu za Afya unaonesha kuwa, vifo vilivyotokana na matumizi ya mihadarati aina ya afyuni (opiods) miongoni mwa wazee wenye zaidi ya miaka 65 viliongezeka kwa asilimia 53 mwaka 2020 nchini Marekani.
Aidha kwa mujibu wa utafiti huo, idadi ya vifo vinavyotokana na unywaji wa kupundukia wa pombe baina ya wazee wa Marekani wenye umri uliotajwa iliongezeka kwa asilimia 18 mwaka huo.
Mamlaka za Marekani zimeeleza wasiwasi wao kuhusu ongezeko la vifo vya wazee kutokana na mihadarati na vileo. Dakta Frederic Blow, Profesa wa saikolojia na Mkurugenzi wa Kituo cha Kuwarekebisha Waraibu wa Mihadarati katika Chuo Kikuu cha Michigan ameashiria suala hilo na kusema, "tabaka la wazee wanaotumia mihadarati aghalabu limejificha na pia limepuuzwa."
Takwimu za serikali ya Washington zinaonesha kuwa, karibu wazee milioni moja nchini Marekani wana matatizo ya kisaikolojia kutokana na matumizi ya mihadarati, ambapo asilimia 3 miongoni mwao ni waraibu wa bangi.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa, wazee 11,616 walifariki dunia kutokana na athari za unywaji wa pombe mwaka 2020, huku 5,000 wakiaga dunia kwa kubugia vidonge vingi ambavyo hawajaandikiwa na daktari.
Takwimu za Kituo cha Kudhibiti Magonjwa nchini Marekani CDC zinaonesha kuwa, idadi ya watu wanaopoteza maisha kutokana na matumizi ya mihadarati nchini humo imeongezeka na kupindukia watu laki moja kwa mwaka. Matumizi ya mihadarati nchini Marekani yanaisababishia nchi hiyo hasara ya dola bilioni 740 kila mwaka, mbali na kuchangia pakubwa ongezeko la vitendo vya uhalifu na ajali za barabarani nchini humo.