Argentina yatinga fainali Kombe la Dunia; ndoto za Messi kutimia?
(last modified Wed, 14 Dec 2022 04:26:12 GMT )
Dec 14, 2022 04:26 UTC
  • Argentina yatinga fainali Kombe la Dunia; ndoto za Messi kutimia?

Timu ya taifa ya soka ya Argentina imetinga hatua ya fainali ya mashindano ya soka ya Kombe la Dunia yanayoendelea nchini Qatar baada ya kuibamiza timuu ngumu ya Crotia mabao 3 kwa nunge.

Kwa ushindi huo sasa Argentina inasubiria mshindi wa leo kati ya Morocco na mabingwa watetezi Ufaransa ili kupepetena katika hatua ya fainali.

Yalikuwa ni magoli mawili yaliyowekwa kimiani na mshambuliaji Julian Alvarez, yakitanguliwa na mkwaju wa penalti kutoka kwa nahodha Messi ulio

Wachezaji wa timu ya soka ya taifa ya Argentina wakishangilia moja ya mabao katika mchuano wa nusu fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Croatia

 

tingisha nyavu za Croatia katika dakika ya 39 vilivyozusha shamrashamra na sherehe si uwanjani Lusail tu mjini Doha, bali kote nchini Argentina, ambako maelfu ya mashabiki wamejitokeza mitaani kumtukuza shujaa wao, Messi, kwa kuiongoza timu yao ya taifa kwa ushindi wa 3-0 dhidi ya Croatia na hivyo kujikatia tiketi ya moja kwa moja kuelekea fainali.

Baada ya mechi hiyo, Messi aliwaambia waandishi wa habari kwamba moyo wake umejaa mchanganyiko wa furaha na hamasa kuwaona wale aliowaita familia yake, akimaanisha mashabiki, "wakipeperusha bendera za nchi yao kwa furaha ya ushindi."

"Muhimu kuliko yote ni kwamba sasa tunakwenda kwenye fainali na hicho ndicho hasa tulichokuwa tunakitaka." Alisema nahodha huyo wa Argentina.

Lionel Messi ambaye anatajwa kama mchezaji mwenye kipaji cha pekee katika kuusakata kabumbu hajawahi kushinda Kombe la Dunia licha ya kupata zawadi na tuzo kemkemu nyingine. Wengi wanajiuliza je mara hii nguli huyo wa soka atatimiza ndoto yake?