Dec 26, 2022 11:48 UTC
  • Erdogan: Ronaldo alikalishwa benchi Kombe la Dunia kutokana na uungaji mkono kwa Palestina

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amedai kuwa nyota wa soka wa Ureno Cristiano Ronaldo alipigwa marufuku ya kisiasa wakati wa michuano ya Kombe la Dunia ya FIFA ya 2022 iliyomalizika hivi karibuni nchini Qatar kwa kuunga mkono Palestina.

Akizungumza katika hafla na vijana katika jimbo la Erzurum mashariki mwa nchi hiyo siku ya Jumapili, rais wa Uturuki amesema Ronaldo "alifujwa" katika Kombe la Dunia.

Walimfuja Ronaldo. Kwa bahati mbaya, wamempiga marufuku ya kisiasa. Kumpeleka mwanasoka kama Ronaldo uwanjani zikiwa zimesalia dakika 30 tu kabla ya mechi kumalizika kuliharibu saikolojia yake na kumwondolea nguvu,” Erdogan amesema.

"Ronaldo ni mtu ambaye anasimama kwa ajili ya Palestina," ameongeza Rais wa Uturuki wakati akimlinganisha mwanasoka huyo wa Ureno na Lionel Messi wa Argentina.

Mshambuliaiji huyo nyota alipumzishwa katika kipindi cha kwanza cha mechi ya Ureno katika robo fainali ya Kombe la Dunia 2022 dhidi ya Morocco na alifika uwanjani kipindi cha pili, jambo lililowasikitisha mashabiki wa soka wa Ureno.

Ronaldo, mwanasoka wa kwanza wa kiume wa kimataifa kufunga bao kwenye michuano mitano ya Kombe la Dunia, alionekana akitoka uwanjani akilia baada ya timu yake kutolewa na Morocco.

Alikuwa ameondolewa kwenye kikosi kilichoanza kwa mechi ya Ureno dhidi ya Uswizi katika hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia, akitokea kama mchezaji wa akiba. Mchezaji huyo wa zamani wa Manchester United na Real Madrid anajulikana kama muungaji mkono wa Palestina.

 

Tags