Mar 11, 2024 08:15 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Machi 11

Hujambo mpenzi msikilizaji, natumai u bukheri wa afya. Karibu tutupie jicho baadhi ya matukio makubwa ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbalimbali za dunia...

Iran bingwa uendeshaji mitumbwi

Timu ya taifa ya wanawake ya Iran imetwaa ubingwa wa Mashindano ya Kuendesha Mitumbwi Mtoni ya Asia kwa mwaka huu 2024. Akina dada hao wa Iran wameibuka kidedea kwenye mashindano hayo ya Asian River Rafting Championships yaliyofanyika huko Himachal Pradesh, kaskazini mwa India. Jitihada za Saba Fadaei, Faezeh Ronasi, Sahar Ghasemi Toudeshki, Melina Ebrahimian na Setareh Homayoon Fard zimeifanya timu hiyo ya wanawake ya Iran itawazwe washindi wa kuzoa jumla ya alama 300 na kutunukiwa medali ya dhahabu.

 

Timu C ya India imeshinda medali ya fedha baada ya kuibuka ya pili kwa alama 262, huku orodha ya tatu bora kwenye mashindano hayo ya kieneo ikifungwa na Timu C tena kwa kuchota alama 242, mbele ya Timu ya B ya India.

Polo ya majini; Iran yaibuka ya 2

Iran imeibuka mshindi wa pili kwenye mashindano ya polo ya majini ya vijana wa Asia ya mwaka huu 2024. Siku ya Jumamosi vijana wa Iran walishindwa kufurukuta mbele ya Japan kwenye mchezo wa fainali na kuishia kuzabwa magoli 17-13. Timu hiyo ya mpira wa polo wa wachezaji saba kila upande inayonolewa na Ali Pirouzkhah, ilizishinda Malaysia, Sri Lanka, Singapore, Kazakhstan na China kabla ya kutinga fainali. Vijana hao wa Kiirani mbali na kutunukiwa medali ya fedha kwenye mashindano hayo, lakini pia wamejikatia tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa ya World Aquatics Men’s U18 Water Polo Championships yatayofanyika baadaye mwaka huu nchini Argentina. Mashindano hayo ya Asian Age Group Championship yaliyofanyika baina ya Februari 26 na Machi 9 katika Ukumbi wa New Clark City Aquatics Center huko Capas, mjini Tarlac, nchini Ufilipino, umevutia wanamichezo zaidi ya 1,000 kutoka nchi 25 za Asia.

 

Mapema Jumamosi, Kazakhstan ilitunukiwa medali ya shaba baada ya kuishinda China kwa alama 7-4 katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu.

Kadhalika Iran imeibuka bingwa kwenye mashindano ya mieleka ya freestyle ya Yasar Dogu 2024 yaliyofanyika nchini Uturuki. Iliibuka kidedea Jumapili kwenye mashindano hayo baada ya kuzoa medali 3 za dhahabu, na 2 za fedha.

Wakati huohuo, Iran imezoa medali lukuki kwenye mashindano ya mieleka ya Dan Kolov-Nikola Petrov yaliyofanyika mjini Sofia, Bulgaria baina ya Machi 7-11, 2024.

Mashindano ya All African Games yaanza

Duru ya 13 ya Mashindano ya Afrika ya 'All African Games'ilizinduliwa rasmi Ijumaa ya Machi 8 jijini Accra, Ghana. Rais wa Ghana, Nana Akufo Addo aliongoza uzinduzi wa mashindano hayo, huku yakiwashirikisha wanamichezo kutoka mataifa 54 ya Afrika. Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania, Hamis Mwinjuma wa Tanzania ameongoza timu ya wanamichezo kutoka nchi hiyo ya Afrika Mashariki, watakaochuana na wachezaji wa mataifa mengine katika mchezo wa kriketi wanawake, mpira wa miguu wanawake chini ya miaka 20, Judo, riadha, kuendesha baiskeli na kuogelea.

Siku ya Alkhamisi, timu ya taifa ya soka ya vijana ya Uganda 'Hippos' iliiadhibu Nigeria mabao 2-1 katika mchezo wao wa ufunguzi jijini Accra. Kocha wa Hippos, Morley Byekwaso amesema wangeliumia moyo sana iwapo wangefungwa kwenye mchezo huo kwa kuzingatia kuwa walitandikwa na Nigeria walipokutana mwaka jana.

 

Katika mchuano mwingine wa Kundi B, Senegal iliitandika Sudan Kusini bao 1-0. Nayo timu ya wanawake wenye chini ya miaka 20 ya Ghana iliizaba Ethiopia bao 1-0. Nigeria Falconets iliisasambua Morocco mabao 2-0 katika mechi za wanawake wenye chini ya miaka 20.

Wenyeji Ghana wamekwea hadi nafasi ya 7 kwenye jedwali la medali kwa kuzoa medali nne ikiwemo ya dhahabu, huku Nigeria ikitamalaki kwa medali 8, Senegal (6) na Madagascar (7), ingawaje timu zote hizo, ghairi ya Ghana hazina medali ya dhahabu.

Dondoo za Hapa na Pale

Droo ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho la Shirikisho la Soka Afrika CAF inatazamiwa kuchezwa Jumanne hii ya Machi 12 katika mji mkuu wa Misri, Cairo. Timu zilizofuzu hatua ya robo fainali 2023/24 ya CAF Champions League ni; Yanga na Simba za Tanzania, Petro Luanda ya Angola, ASEC Mimosas ya Ivory Coast, TP Mazembe ya DRC, Al Ahly ya Misri, na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini. Zilizofuzu kwa robo fainali ya Confederation Cup ni USM Alger (Algeria), Zamalek (Misri), Dreams FC (Ghana), RS Berkane (Morocco), Modern Future (Misri), Abu Salem (Libya), Rivers United (Nigeria) na Stade Malien (Mali).

Kwengineko, bondia nyota wa kimataifa, Francis Ngannou mzaliwa wa Cameroon licha ya kupoteza pambano muhimu Ijumaa dhidi ya bingwa wa uzani mzito duniani Anthony Joshua, lakini amefanikiwa kuvuna kiasi cha dola milion 20. Kiwango hiki ni kikubwa zaidi ya kile alichowahi kukusanya kwenye michezo ya UFC kwa miaka saba, ambapo alivuna dola milioni 3.5. Katika mapambano mawili aliyopigana dhidi ya Tyson Fury na Antony Joshua, Ngannou mwenye umri wa miaka 37 amekusanya jumla ya dola milioni 30. Joshua ametia kibindoni dola milioni 50 kwa ushindi huo wa aina yake baAda ya pambano la raundi 2 lililodumu kwa takriban dakika 6 Ijumaa.

Na katika Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, wachezaji nyota wa Arsenal Declan Rice na Kai Havertz walifunga mabao muhimu katika dakika za 19 na 86 mtawalia katika mchezo wa wikendi dhidi ya Brentford ulioshia kwa Gunners kuvuna ushindi wa mabao 2-1 na na kukwea hadi kileleni mwa jedwali la EPL. Wenyeji Arsenal walitinga Emirates Jumamosi wakiwa chini ya shinikizo la kushinda ili kujaribu kuhepa mbanano ulioko katika nafasi tatu za kwanza, timu hizo nyingine mbili zikiwa ni Liverpool na Manchester City. Arsenal walipata bao la kwanza kupitia kwa Declan Rice kunako dakika ya 19. Hata hivyo kabla ya kukamilika kwa kipindi cha kwanza, Yoane Wissa alisawazishia Brentford kunako dakika nne za ziada zilizoongezwa baada ya 45 za kwanza. Baada ya mapumziko timu hizo ziliendelea kushambuliana ambapo vijana wa Arteta wakapata bao la ushindi ambalo lilijazwa kimiani na Kai Havertz katika dakika ya 86 ya mchezo.

Kai Havertz akishangilia bao lake

 

Siku ya Jumapili Liverpool ilimkaribisha nyumbani Manchester City. Miamba hiyo hiyo miwili ilikabana koo katika Uwanja wa Anfield wenye uwezo wa kubeba mashabikia 60,000 na kuambulia sare ya kufungana bao 1-1. Wageni City walitangulia kuona lango la wenyeji kwa bao la John Stones katika dakika ya 23. Liverpool ilifanya mambo kuwa sawa bin sawa kwa bao la dk 50 lililotiwa kimyani na Alexis Mac Allister kupitia mkwaju wa penati.

Liverpool uwanjani

 

Manchester United pia Jumamosi iliambulia ushindi wa mabao 2-0 iliposhuka dimbani kuvaana na Everton nyumbani Old Trafford. Mashetani Wekundu walipata mabao yao kupitia mikwaju ya penati iliyofungwa na Bruno Farnandes na Marcus Rashford katika kipindi cha kwanza.

Arsenal wanaongoza jedwali la EPL kwa alama 64 mbele ya Liverpool ambao pia wamefikisha alama 64, lakini wanazidiwa kwa wingi wa magoli la Gunners, huku City wakifunga tatu bora kwa alama 63. Mashetani hao wametulizana katika nafasi ya sita wakiwa katika alama 47. Baada ya raundi ya 28 ya EPL, ligi hiyo sasa itasimama kwa wiki tatu kupisha michezo ya Kombe la FA na mechi za mataifa. EPL itarejea Machi 30, ambapo vinara Arsenal watakuwa Etihad kuvaana na Manchester City, na Liverpool watakuwa Anfield kuwaalika Brighton.

 

Tags