May 04, 2024 02:32 UTC
  • M23 wadai kuuteka mji wenye madini muhimu wa Rubaya, mashariki ya DRC

Kundi la waasi la M23 ambalo linadaiwa kuwa na uhusiano na Rwanda limetangaza kwamba, limeuteka mji wa Rubaya ulioko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambao ni maarufu kwa madini muhimu yanayotumika katika utengenezaji wa simu za kisasa za mkononi.

Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari, msemaji wa kundi hilo amesema, mji huo wa Rubaya "umekombolewa."
 
Kwa upande wake, Jeshi la Kongo DR limekataa kutoa maelezo yoyote kuhusu dai hilo la waasi.
 
Mji wa Rubaya una akiba kubwa ya madini ya coltan, yanayotoa 'tantalum' inayotumika sana katika utengenezaji wa simu za kisasa za mkononi 'simuerevu'. Ni miongoni mwa madini ambayo yalitajwa mapema mwezi huu katika barua iliyoandikwa na Serikali ya Kinshasa kuihoji Kampuni ya Apple juu ya taarifa ilizonazo kuhusu kile kilichotajwa kuwa ni "madini ya damu" yanayosafirishwa kupitia mkondo wa usambazaji wa kampuni hiyo.
 
Mapigano yamepamba moto katika miezi ya hivi karibuni kati ya waasi wa M23 na vikosi vya jeshi la Kongo, wakati Umoja wa Mataifa ukiwa unapanga kuwaondoa askari wake wa kulinda amani katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo ifikapo mwisho wa mwaka huu.
Kushoto ni Rais Felix Tshisekedi wa DRC

Onesphore Sematumba, mchambuzi wa Kundi la Kimataifa la Migogoro (International Crisis Group) amesema, kutekwa kwa Rubaya ni mabadiliko makubwa na muhimu katika mgogoro wa DRC.

Sematumba amevieleza vyombo vya habari kuwa, Rubaya ina akiba nyingi ya madini na bila shaka kutekwa kwake kutaipa M23 fursa ya kufaidika na madini hayo.

Wakati huohuo, John Banyene, mwanaharakati wa mashirika ya kiraia ameziambia duru za habari kwamba waasi wa M23 wanasonga mbele kuelekea Goma, ambao ni mji mkubwa zaidi wa mashariki mwa Kongo na mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.

Mgogoro wa miongo kadhaa wa mashariki mwa Kongo DR umesababisha moja ya hali mbaya zaidi za kibinadamu duniani, huku makundi zaidi ya100 yenye silaha yakipambana kuwania udhibiti wa eneo hilo lenye utajiri wa madini lililoko karibu na mpaka wa pamoja na Rwanda.

Makundi mengi ya wabeba silaha yanatuhumiwa kufanya mauaji ya halaiki, ubakaji na ukiukaji mwingine wa haki za binadamu. Vita na mapigano hayo yamesababisha watu wapatao milioni saba kuyahama makazi yao, wengi wao wakishindwa kufikiwa na misaada.
 
Harakati ya Machi 23 au kwa kifupi M23, ni kundi la kijeshi la waasi linaloundwa na waasi wa kabila la Tutsi ambao walijitenga na jeshi la Kongo DR zaidi ya miaka kumi iliyopita. Waasi hao walifanya mashambulizi makubwa mwaka 2012 na kuidhibiti Goma, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini karibu na mpaka na Rwanda, ambao sasa hivi wanakaribia kuuteka tena.../

 

Tags