Mapigano makali yaibuka tena kati ya jeshi la Kongo na M23
Mapigano makali yameibuka baina ya wanajeshi wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Kundi la waasi wa M23, licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyotiwa saini mwezi uliopita wa Julai.
Aidha mapigano hayo mapya yameripotiwa baada ya makubaliano mengine ya amani kutiwa saini kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Jirani yake Rwanda mjini Washington mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.
Ni Dhahiri kwamba, makubaliano hayo hayajazuia pande hasimu kushambuliana. Kuanzia siku ya Ijumaa wiki iliyopita mapigano yalishuhudiwa katika mji wa Mulamba katika jimbo la Kivu Kusini.
Kulingana na duru za usalama za eneo hilo, M23 iliwafurusha wanamgambo wengine pamoja na wanajeshi wa serikali waliokuwepo katika mji huo baada ya kushambuliana vikali.
Katika taarifa yake, msemaji wa M23 Lawrence Kanyuka, ameishutumu serikali ya Kongo kupanga mashambulizi yaliyo na nia ya kutanua mgogoro uliopo.
Tangu M23 ilipoibuka tena mwaka 2021, wamedhibiti maeneo kadhaa muhimu mashariki mwa Kongo, ikiwemo mji wa Goma mwezi Januari na Bukavu mwezi Februari mwaka huu.
Wakati huo huo, kundi la waasi wa M23 wanaodhibiti maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamekanusha madai ya kuwauwa raia katika jimbo la Kivu Kusini pamoja na madai ya kuajiri askari watoto.
Hivi majuzi Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa, waasi wa M23 waliua watu zaidi ya 300 katika mwezi uliopita wa Julai katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk, alilikosoa kwa matamshi makali kundi la waasi wa M23 linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda kwa mauaji ya takriban watu 319 mashariki mwa DRC mwezi Julai.