Asasi za kiraia, wapinzani wataka kuachiwa huru kinara wa upinzani Congo Brazzaville
(last modified Sat, 17 May 2025 10:28:11 GMT )
May 17, 2025 10:28 UTC
  • Asasi za kiraia, wapinzani wataka kuachiwa huru kinara wa upinzani Congo Brazzaville

Vyama vya siasa, mashirika ya kutetea haki za binadamu na asasi za kiraia zimeedelea kushinikiza kuachiwa huru kinara wa upinzani nchini Congo Brazzaville, anayedaiwa kutekwa nyara hivi karibuni.

Lassy Mbouity, kiongozi wa chama cha upinzani cha Les Socialistes Congolais na ambaye pia mgombea katika uchaguzi wa rais wa Machi 2026 nchini Congo, alitekwa nyara Jumapili iliyopita mjini Brazzaville na watu waliokuwa na silaha na waliofunika nyuso zao - siku chache baada ya kunusurika katika jaribio la mauaji.

Chama chake kinailaumu serikali kwa utekaji huo. Kisema, "Tuna hakika kuwa ni serikali ya kidikteta ya Brazzaville inayoongoza hili. Hii si mara ya kwanza. Alikamatwa huko nyuma, na watu waliofika nyumbani kwake walikuwa wamefunikwa nyuso, wakiwa na silaha, na wakitumia gari lisilo na nambari za usajili. Ndiyo maana tunaamini kuwa huo ni utekaji nyara."

"Tunapanga kuendelea kuhamasisha - sio tu miongoni mwa wanasoshalisti bali miongoni mwa wananchi wote wa Congo," Martial Mbourangon Pa’nucci, msemaji wa chama cha Les Socialistes Congolais amesema. Baadhi ya vyama vya upinzani vilijiunga na Les Socialistes Congolais kutoa taarifa ya pamoja siku ya Alkhamisi kulaani utekaji huo na kutaka Mbouity aachiliwe bila masharti.

"Kitendo hiki cha woga ni sehemu ya vitendo vya kigaidi vilivyokithiri, vitisho, na ukiukwaji wa haki za binadamu katika Jamhuri ya Congo. Ni ukiukaji mkubwa wa uhuru wa kibinafsi na ukiukaji wa moja kwa moja wa Kifungu cha 9 cha Katiba ya Oktoba 25, 2015. Tunataka Lassy Mbouity aachiliwe huru mara moja." Clément Mierassa, mkuu wa Chama cha Kidemokrasia cha Kongo, alisema.

Shirika la Haki za Kibinadamu la Kongo pia limejiunga na miito hiyo ya kutaka kuachiwa huru mwanasiasa huyo, ambapo limewasilisha ombi la dharura kwa wanadiplomasia na mashirika ya kimataifa kuingilia kati. Serikali ya Brazzaville bado haijatoa taarifa rasmi kuhusu tuhuma hizo za utekaji nyara.

Hivi karibuni, vyama vitatu vya upinzani vya Congo Brazzaville viliunda muungano kabla ya uchaguzi wa 2026. Shabaha kubwa ya muungano huo ni kumuondoa madarakani Rais Denis Nguesso, ambaye amekuwa akiitawala nchi hiyoi tangu mwaka 1997.