May 04, 2024 03:14 UTC
  • Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Audrey Azoulay
    Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Audrey Azoulay

Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO), limetoa tuzo yake ya mwaka kwa waandishi wa habari wa Gaza, kwa mnasaba wa Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani.

Tuzo hiyo imetolewa na UNESCO kwa waandishi wa habari wa Ukanda wa Gaza wanaoripoti vita vya Israel dhidi ya watu wa eneo hilo la Palestina.

Katika taarifa yake, UNESCO imesisitiza kuwa kutolewa tuzo hii kwa waandishi wa habari wa Gaza kunaonyesha ukweli kwamba, uhuru hatimaye utapatikana kwa waandishi wa habari wa Palestina.

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, hadi sasa zaidi ya waandishi wa habari 140 wa Kipalestina wameuawa shahidi wakiripoti au kutayarisha habari za mashambulizi ya kinyama ya Israel dhidi ya raia wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.

Mkuu wa Jumuiya ya Waandishi wa Habari wa Palestina, Nasser Abu Bakr, alipokea tuzo hiyo kwa niaba ya waandishi habari wa Gaza katika hafla iliyofanywa na UNESCO Ijumaa ya jana katika mji mkuu wa Chile, Santiago, katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, inayosadifiana na Mei 3 ya kila mwaka. 

Katika hotuba yake baada ya kupokea tuzo hiyo, Abu Bakr amekutaja kutolewa tuzo hiyo kwa waandishi wa habari wa Gaza kama "tukio kubwa la kihistoria", lakini alidokeza kuwa furaha ya kupata tuzo hiyo imechanganyika na masikitiko ya kupoteza mashahidi wa vyombo vya habari vya Palestina.

Mkuu wa Jumuiya ya Waandishi wa Habari wa Palestina amesisitiza "nia na nazma ya kuwawajibisha viongozi wa Israel wanaoendelea kuua raia wasio na hatia wa Palestina na kuwafungulia mashtaka."

Abu Bakr ametoa wito kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), Karim Khan, kuanza haraka taratibu za uchunguzi wa uhalifu wa Israel wa kuua zaidi ya waandishi habari 140 katika eneo la Ukanda wa Gaza.