Mar 04, 2024 07:20 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Machi 4

Natumai hujambo mpenzi msikilizaji. Karibu tuangazie baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyoshuhudiwa ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa, kieneo na kimataifa.....

Choopan wa Iran atwaa tuzo ya kifahari

Mtunishaji misuli veterani wa Iran, Hadi Choopan ametwaa taji la kimataifa la 'Bwana Olympia' katika tuzo za Arnold Classic 2024. Fainali ya Arnold Classic ilifanyika Jumamosi ya Machi 2 katika Ukumbi wa Battelle Grand katika mji wa Columbus jimboni Ohio, magharibi ya Marekani. Choopan mwenye umri wa miaka 36 ametunukiwa medali ya dhahabu na kitita cha dola 300,000 pesa taslimu baada ya kuibuka kidedea kwenye mashindano hayo ya kimataifa. Muirani huyo mwenye lakabu ya "Persian Wolf" amempiga na chini bingwa mtetezi Samson Dauda kwenye fainali. Choopan ametunukiwa tuzo hiyo ya kifahari na muigizaji maarufu wa Hollywood, Arnold Schwarzenegger. Bingwa huyo wa utunishaji misuli wa Iran anatazamiwa kurejea mjini Las Vegas jimboni Nevada, kwenye michuano ya 'Mr Olympia' baina ya Oktoba 10 na 13 mwaka huu 2024.

Choopan na Arnold Schwarzenegger

 

Wakati huo huo, Ahmad Aminzadeh wa Iran ndiye bingwa wa mchezo wa kunyanyua uzani mzito duniani kwa upande wa walemavu. Alitunukiwa medali ya dhahabu baada ya kuibuka kidedea kwenye Duru ya 13 ya Mashindano ya Dunia ya Mabingwa wa Unyanyuaji Uzani ya Fazza huko Dubai, Imarati. Alinyanyua uzani wa kilo 267 katika jaribio lake la tatu, baada ya kunyanyua kilo 250 na 260 katika jaribio la kwanza na la pili kwa usanjari huo.

Michezo ya Majeshi; Iran ya 2

Timu ya mchezo wa kupiga mishale ya Jeshi la Iran imeibuka ya pili na kutunukiwa medali ya fedha katika Michezo ya Kimataifa ya Majeshi ya mwaka huu 2024 yaliyofanyika huko Bangladesh. Sadegh Ashrafi, Mohammad-Hossein Golshani, na Reza Shabani waliliwakilisha Jeshi la Iran katika safu ya 'archery' kwenye mashindano hayo ya dunia.

Iran ilishindwa kufurukuta mbele ya Korea Kusini kwenye fainali ya kategoria ya recurve bow na kutunukiwa medali ya fedha. Kabla ya hapo, Iran iliibuka kidedea dhidi ya Sri Lanka kwa kuambulia alama 6-0 na Russia kwa pointi 6-2.

Magongo ya theluji; Iran yatupwa nje

Timu ya taifa ya mchezo wa magongo ya kwenye theluji ya Iran imebanduliwa nje ya Mashindano ya Dunia ya World Championships Division III yaliyofanyika huko Sarajevo, Bosnia and Herzegovina. Hii ni baada ya kuzabwa alama 8-5 na Singapore kwenye mchezo wake wa tano wa Kundi B. Kabla ya hapo, Iran ilichapwa na Bosnia (3-0), Ufilipino (14-2), Korea Kaskazini (9-4), na Hong Kong (11-3).

 

Mwenyeji Bosnia and Herzegovina imesogea mbele kwenye michuano ya Kundi A, itakayopigwa Bishkek, Kyrgyzstan kuanzia Machi 10-16. Mechi za Kundi B zilichezewa katika Ukumbi wa Skenderija Sports Arena in Sarajevo, Bosnia and Herzegovina baina ya February 23-29.

CAF; Simba na Yanga zatinga robofainali

Kwa mara ya Kwanza katika historia klabu za Yanga na Simba zimeweka rekodi ya Tanzania kuingiza timu mbili kwenye hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye msimu mmoja. Yanga imefanikiwa kusogea mbele licha ya kulimwa bao 1 bila jibu ugenini na al-Hilal katika Uwanja wa Kimataifa wa Cairo. Bao la Waarabu kwenye mchuano huo wa Kundi B lilitiwa kimyani na Hussein el-Shehat kunako dakika ya 46 ya mchezo. Kitendo cha kumaliza katika nafasi ya pili baada ya kufungwa bao 1-0 na al-Ahly huko Cairo, Misri kinaifanya klabu hiyo ya Tanzania imalize ikiwa nafasi ya pili kwenye kundi D na pointi zake nane, nyuma ya al-Ahly ambayo ni kinara ikiwa na pointi 12.

 

Klabu ya Simba wikendi ya wiki iliyopita ilitangulia hatua ya Robo Fainali, kwenye Michuano ya Klabu Bingwa Afrika kwa mara ya kwanza katika historia tangu kuanzishwa kwake mwaka 1935, baada ya kuinyoa kwa chupa, tena bila maji CR Belouizdad ya Algeria, kwa kuizaba mabao 4-0 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.  Aidha wikendi hii, Simba ilichuana na Jwaneng Galaxy na mchezo kuishia kwa Wekundu wa Msimbazi kuwalisha wageni mabao 6-0 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam. Mbali na Simba na Yanga za Tanzana, timu nyingine zilizofuzu hatua ya Robo Fainali 2023/24 ya CAF Champions League ni; Petro Luanda ya Angola, ASEC Mimosas ya Ivory Coast, TP Mazembe ya DRC, Al Ahly ya Misri, na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Riadha: Kipchoge abwagwa

Mwanariadha kinda wa Kenya, Benson Kipruto amelambisha sakafu veterani Eliud Kipchoge akitawala mbio za Tokyo Marathon nchini Japan, Jumapili, Machi 3. Katika raundi hiyo ya kwanza ya Marathon Kuu Duniani (WMM), bingwa wa Boston Marathon 2021 na Chicago Marathon 2022 Kipruto alikata utepe wa kwanza baada ya kukamilisha umbali huo wa kilomita 42 kwa saa 2:02:16. Muda wake bora katika 42km ulikuwa 2:04:02 kutoka Chicago Marathon 2023 kwa hivyo ameuimarisha kwa dakika moja na sekunde 46. Mbali na kupata muda wake bora mpya, Kipruto, 32, pia alifuta rekodi ya Tokyo Marathon ya 2:02:40 ambayo Kipchoge aliweka mwaka 2022 akishinda makala ya 2021. Alifuatwa kwa karibu na Wakenya Timothy Kiplagat (2:02:55) na Vincent Ngetich (2:04:18) walioimarisha muda wao kutoka 2:03:50 na 2:03:13, mtawalia. Kipchoge, ambaye anashikilia muda bora dunia kwa watimkaji walio hai wa saa 2:01:09 baada ya mshikilizi wa rekodi ya dunia Kelvin Kiptum (2:00:35) kufariki Februari 11, 2024 alitarajiwa kufanya vyema. Hata hivyo, mtimkaji huyo mwenye umri wa miaka 39, ambaye ni bingwa mara mbili wa Olimpiki na ameshinda WMM mara tano, aliambulia nafasi ya 10 kwa saa 2:06:50.

Kipchoge mara hii aonyeshwa kivumbi na wanariadha chipukizi

 

Katika hatua nyingine, mwariadha nyota wa Kenya aliyeaga dunia hivi karibuni, Kelvin Kiptum ameshinda Tuzo ya Mwanariadha Bora wa Mwaka SOYA kwa mwaka 2023. Katika hafla ya utoaji tuzo iliyofanyika Ijumaa katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa KICC jijini Nairobi, Kiptum alitawazwa kuwa mwanariadha bora wa mwaka kwa kiume, huku Patrick Makau, ambaye amewahi kushikilia rekodi ya kuvunja rekodi ya marathon akipokea tuzo hiyo kwa niaba ya mwendazake.  Kiptum alifariki dunia akiwa na miaka 24 katika ajali akiwa na kocha wake Gervais Hakizimana mnamo Februari 11. Alizikwa kaunti ya Elgeyo Marakwet Ijumaa ya Februari 23, katika mazishi yaliyowaleta pamoja viongozi wa hadhi ya juu serikalini na duniani, akiwemo Rais William Ruto. Tuzo ya Mwanariadha Bora wa Mwaka kwa mwaka 2023 kwa upande wa wanawake imemuendelea Faith Kipyegon ambaye pia hakuwepo ukumbuni KICC wakati wa utoaji wa tuzo hizo.

Dondoo za Hapa na Pale

Rais wa Shirikisho la Soka Duniani FIFA, Gianni Infantino ameipongeza timu ya taifa ya soka ya ufukweni ya Irankwa kuibuka mshindi wa tatu katika mashindano ya dunia ya soka ya ufukweni 'Beach Soccer' huko Dubai, Imarati. Iran ilitunukiwa medali ya shaba katika fainali za Kombe la Dunia la Shirikisho la Kandanda Duniani FIFA, baada ya kuichabanga Belarus mabao 6-1 katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu mnao Februari 25.

Rais wa FIFA, Gianni Infatino

 

Kwengineko, Baraza la Soka la Muungano wa Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limeiteua Zanzibar kuwa mwenyeji wa mashindano yajayo ya Kombe la Chalenji mwaka huu 2024. Hayo yalitangazwa Ijumaa hii huko Mombasa Kenya na Isayas Jiran, Makamu wa Rais wa CECAFA ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati Andalizi ya Mashindano. Tangazo hilo limepokewa kwa moyo mkunjufu na Suleiman Mahmoud Jabir, Rais wa Shirikisho la Soka Zanzibar ZFF.

Na kwenye Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, klabu ya Manchester United siku ya Jumapili ilidhalilishwa na jirani yake Manchester City kwa kugaragazwa mabao 3-1 katika mchezo wa EPL uliopigwa katika uwanja wa Etihad. Na kama wanavyosema daima, kutangulia sio kufika, City walitoka nyuma na kuwadhalilisha Mashetani Wekundu ambao hadi wanaenda mapumzikoni, walikuwa kifua mbele kwa goli la mapema la Marcus Rashford la dakika ya 8. Hata hivyo City walirejea kipindi cha pili kwa ari na kasi ya juu, na kuichabanga United mabao 3 yaliyofungwa na Phil Foden (56,80) huku Earling Halaand akilizamisha kabisa jahazi la mashetani. Ushindi huo umeipelekea City hadi katika nafasi ya pili ya msimamo wa EPL kwa alama 62, na sasa watasafiri hadi Anfield Machi 10 kuwavaa Liverpool.

.………..TAMATI…………

Tags