Ulimwengu wa Spoti, Feb 2
Hujambo msikilizaji mpenzi na karibu tutupie jicho matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa, kieneo na kimataifa.
Futsal Asia; Iran yaanza vizuri
Timu ya taifa ya futsal ya Iran imeendelea kutetea taji lake kwa kuvuna ushindi mfululizo katika mechi zake za utangulizi. Iran iliishukia vibaya Afghanistan siku ya Jumapili katika mchuano wa Kundi D la Kombe la Futsal la Asia 2026 kwa ushindi wa mabao 5-2. Vijana wa Iran walilazimika kujituma zaidi katika mchuano huo ili wajikatie tiketi ya robo fainali, wakifahamu fika kuwa Afghanistan si lele mama.

Kabla ya hapo, Iran ilinusurika mtihani mkali na kuishinda Saudi Arabia mabao 2-0 katika mchezo wao mwingine wa Kundi D wa AFC Futsal Asian Cup Indonesia 2026 siku ya Ijumaa. Mabingwa hao watetezi walihimili mashinikizo makubwa kutoka Saudia katika mchezo mzima kabla ya mabao mawili ya kipindi cha pili kuwaweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele hadi hatua ya mtoano. Aidha Iran kabla ya hapo iliibinjua Malaysia mabao 4-1 katika mchezo mwingine wa Kundi D wa mashindano hayo ya kibara ya Kombe la Asia la Futsal yaliyoandaliwa na Shirikisho la Futsal Asia AFC ya 2026 huko Indonesia. Afghanistan pia, hapo awali ilifuzu kwa robo fainali kwa ushindi dhidi ya Saudi Arabia na Malaysia katika kundi hilo. Mabingwa watetezi - ambao walimaliza na pointi tisa - watakabiliana na Uzbekistan katika robo fainali huku Afghanistan ikicheza na Japan.
Judo: Iran yazoa dhahabu
Bingwa wa Judo, Elyas Parhizgar wa Iran alishinda medali ya dhahabu katika kundi la majudoka wenye uzito wa kilo 81 katika Mashindano ya Casablanca African Open 2026 yaliyofanyika nchini Morocco. Parhizgar ilimshinda Konin Junior Emmanuel Kossan kutoka Côte d'Ivoire na kisha Ivan Ferreira kutoka Argentina katika mapambano yake ya awali. Kadhalika alimshinda Siem Van Damme kutoka Uholanzi na kutinga robo fainali na kisha kumshinda Mustafa Habib kutoka Bosnia Herzegovina na kutinga nusu fainali. Katika nusu fainali, Parhizgar alipata ushindi muhimu dhidi ya Olivier Gagnon kutoka Canada na kutinga fainali. Ni katika pambano la fainali ya kufa kupona alipomchakaza Antonio Candreio, na kutunukiwa medali ya dhahabu. Muirani mwenza, Amir-Hossein Valizadeh wa safu ya majudoka wenye uzito wa kilo 73 alishindwa na Felix kutoka Canada katika fainali na kuzawadiwa medali ya fedha. Majudoka kutoka nchi 42 duniani, walishiriki mashindano hayo, ambapo timu ya taifa ya Iran, ikiongozwa na Rashad Mammadov, iliwakilishwa na majudoka watano.
Wanamichezo wa Iran wamkingia kifua Kiongozi Muadhamu
Zaidi ya wanachama 5,000 wa jumuiya ya michezo ya Iran wametoa taarifa kulaani vitisho na bwabwaja za Rais wa Marekani Donald Trump, wakitangaza uungaji mkono wao mkubwa kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei. Taarifa hiyo, iliyosainiwa na wanariadha, wakufunzi, maveterani, maafisa wa michezo na akurugenzi leo Jumapili, imelaani vikali matamshi ya vitisho ya Trump, ikiyaita ishara ya kukatishwa tamaa mbele ya umoja na uongozi wa kitaifa wa Iran. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanariadha na wanamichezo wa Iran, wakiongozwa na mafundisho ya Kiislamu na urithi wa mashahidi, wanajitazama kama walinzi wa heshima ya taifa, izza na uhuru wa Jamhuri ya Kiislamu. Imesisitiza kwamba, michezo nchini Iran imejikita katika maadili ya ushujaa, Muqawama, uadilifu na maadili ndani na nje ya uwanja. Wakilaani tishio lolote au matusi dhidi ya uongozi na taifa la Iran, wanamichezo hao wamethibitisha uaminifu wao usioyumba kwa Kiongozi, Muadhamu wakimwelezea Ayatullah Khamenei kama nembo ya umoja na nguvu ya taifa.

Kadhalika wameonya kwamba, hatua yoyote ya uadui dhidi ya mamlaka ya kujitawala au uongozi wa Iran itakabiliwa na jibu kali. Wakihitimisha taarifa hiyo, waliotia saini taarifa hiyo wametangaza utayarifu wao kamili wa kujitolea katika kuilinda Iran, maadili yake ya Kiislamu na maadili ya Mapinduzi, wakisisitiza kwamba historia itahukumu maneno ya vitisho ya Rais wa Marekani, huku watu wa Iran wakiendelea kusimama imara katika kila uwanja.
Soka Afrika
Klabu ya soka ya Simba ya Tanzania imeendelea kuvuta mkia katika michuano ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika. Hii ni baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa nne wa Kundi D uliochezwa Jumapili ya Februari Mosi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Nairobi, walipovaana na Esperance de Tunis ya Tunisia. Shomari Kapombe aliitanguliza Simba SC dakika ya 39, kabla ya Yusuph Kagoma kuongeza bao la pili dakika ya 45.
Hata hivyo, Esperance walifanikiwa kusawazisha kupitia Aboubacar Diakite dakika ya 64 na Kouceilia dakika ya 79. Kiungo wa Simba SC, Yusuph Kagoma, alitangazwa kuwa Mchezaji Bora wa Mechi kutokana na kiwango bora alichokionesha, huku nyota wa Esperance H. Jelassi akikosa nafasi ya kuipatia timu yake bao baada ya kukosa mkwaju wa penalti. Simba SC inaendelea kuburuza mkia baada ya kukusanya pointi moja pekee katika michezo minne ya msimu wa 2025/26. Matokeo hayo yanazidi kuyeyusha ndoto za Wekundu wa Msimbazi za kutinga hatua inayofuata, wakibaki na mechi mbili tu huku wakiwa na pointi kiduchu. Wachambuzi wa spoti wanasema ni muhali kwa Simba SC kufuzu hatua ya robo fainali, hasa iwapo Esperance watafanikiwa kupata matokeo chanya katika mchezo wao ujao. Matokeo ya sare yamewaumiza mashabiki wa klabu ya Simba Sc ambao walijitokeza kushuhudia mchezo huo na baadhi yao kutokana na maamuzi yao ya hasira waliamua kumvamia mwenyekiti wao kwani wanaamini kwamba kiongozi huyo ndiyo chachu ya kuporomoka kwa ubora wa timu yao. Mara baada ya jeshi la Polisi kuingilia kati na kumnusuru kiongozi huyo, Murtaza Mangungu amesikika akieleza wazi kwamba timu ya Simba Sc siyo ya kwake peke yake lakini wakati wote mambo yanapokuwa mabaya kwa maana ya timu inapopata matokeo mabaya lawama zote huwa anapewa yeye peke yake kitu ambacho kinamuumiza.

Watani wao wa jadi, klabu ya Yanga, pia walitoshana nguvu kwa kutoa sare ya bao 1-1 na klabu ya al-Ahly ya Misri katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyopigwa Januari 31 katika Dimba la New Amaan Complex, Zanzibar. Kwa sare hiyo, Al Ahly wakibaki kileleni wakiwa na pointi 8, huku Yanga na wao wakisalia nafasi ya pili kwenye kundi wakiwa na pointi 5. Yanga walitangulia kupata bao kunako dakika ya 41+1’ kupitia bao la Ibrahim Bacca. Waarabu walisawazisha kunako dakika ya 60’ kupitia goli la kiustadi la Aliou Dieng.
Katika mchezo wa Kundi B, AS FAR Rabat ya Morocco ilivuna bao 1-0 iliposhuka dimbani kuvaana na JS Kabylie na kufiisha alama 5 mpaka sasa kundini, mbali na kupanda hadi nafasi ya pili. Far Rabat wana nafasi kubwa ya kushinda kwenye mchezo unaofuata dhidi ya Yanga SC, maana watakuwa wanaupigia nyumbani jijini Rabat. Yanga pia wana alama 5 kwenye msimamo wa Kundi B kufikia sasa.
Huku hayo yakiarifiwa, klabu ya Azam ya Tanzania imezima kabisa matumaini ya klabu ya Nairobi United ya Kenya kusonga mbele kwenye mashindano ya kikanda ya Kombe la Shirikisho la Afrika. Hii ni baada ya kuigaragaza klabu hiyo ya Kenya bao 1-0 katika mchuano wa Jumapili, wiki moja baada ya kuichabanga mabao 2-1 uwanjani Nyayo jijini Nairobi, katika mchuano mwingine wa Kundi B. Bao la mapema la Faisal Salum lilitosha kuwapa Azam alama 3 muhimu katika mechi hiyo iliyopigwa katika Uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar. Azam sasa wana alama 6 kundini wakiwa katika nafasi ya 3, huku Nairobi United wakivuta mkia bila alama. Wydad Casablanca ya Morocco wanaongoza kundi hilo kwa pointi 9, alama sawa na Maniema Union wanaoshika nafasi ya pili, licha ya Maniema ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuvuna ushindi wa mabao 2-1 katika mgaragarazano wao wa karibuni. Mchezo baina ya Singida Black Stars ya Tanania na AS Otoho ya Congo Brazaville ulimalizika kwa vijana wa Singida kulimwa bao 1-0.
Dondoo za Hapa na Pale
Kocha wa timu ya soka ya Manchester City, Mhispania Pep Guardiola kwa mara nyingine ametangaza himaya na uungaji mkono wake kwa Palestina na kusisitiza kwamba, yeye yuko pamoja na Wapalestina. Guardialo amesema hayo katika hafla ya wanaharakati wanaounga mkono Palestina katika pwani ya Barcelona nchini Uhispania na kubainisha kwamba: Ninasema haya wazi kwa kila mtu; Mimi sio kwamba, siko upande wowote, la hasha, bali niko upande wa Wapalestina, ninasimama pamoja na Palestina.

Ninasimama pamoja na wanyonge na wanaokandamizwa, na wanaokandamizwa leo ni Palestina. Katika tukio hilo, meneja huyo wa Manchester City ambaye alikuwa akihudhuria kampeni ya hisani huko Barcelona, alitoa hotuba athirifu kuhusu uhalifu wa utawala wa Israel huko Gaza na kusisitiza umuhimu wa mshikamano wa kibinadamu na waathiriwa wa vita. Amesema…..
INSERT….GUARDIOLA
"Ninapomwona mtoto katika kipindi cha miaka miwili iliyopita akiuliza kupitia picha na vyombo vya habari kuhusu mama yake aliyezikwa chini ya kifusi, nahisi kwamba tumewaacha peke yao; wameachwa na kupuuzwa. Mtoto anauliza: Uko wapi? Njoo utusaidie. Na hadi sasa hatujafanya hivyo." Akihutubia huku akiwa amevaa skafu ya Keffiyeh ambayo ni nembo ya kuonyesha mshikamano na Wapalestina wanaoendelea kuuawa na majeshi ya Israel, kocha huyo wa klabu ya Manchester City ya Uingereza alisisitiza haja ya kutetea na kusimama na wanyonge zaidi, akisema: "Suala hili si la Palestina tu, bali linajumuisha masuala yote ya kibinadamu." Meneja wa Manchester City alisisitiza kwamba lengo la mabomu na ukimya wa kimataifa ni kupuuza ukweli. "Labda ni kwa sababu walio madarakani ni waoga na huwatuma vijana wasio na hatia kuwaua wengine huku wao wenyewe wakifurahia joto au kiyoyozi majumbani mwao. Tunahitaji kupiga hatua mbele, na uwepo wetu pekee una thamani kubwa," aliongeza.
Kwengineko, wananchi wa Senegal wameanzisha kampeni ya kuchanga ili kulipa faini ya dola za Marekani 100,000 aliyopigwa kocha wao Pape Thiaw baada ya fainali ya AFCON 2025 dhidi ya Morocco. Mkufunzi huyo hata hivyo amewashukuru na ameomba michango hiyo wapewe watu wenye uhitaji. Pape Bouna Thiaw ametozwa faini hiyo baada ya kuwaamuru wachezaji kutoka uwanjani. Kwa upande wa Wachezaji, Iliman Cheikh Baroy Ndiaye na Ismaila Sarr wamefungiwa kila mmoja mechi mbili rasmi za CAF kwa tabia mbaya dhidi ya Mwamuzi. CAF pia imelitoza shirikisho la Senegal faini ya dola 300, 000 kwa utovu wa nidhamu wa mashabiki wake na Dola nyingine 300,000 kwa tabia ya utovu wa nidhamu kwa wachezaji wake na timu ya kiufundi. Kwa upande wa Morocco beki nyota Achraf Hakimi amefungiwa kucheza mechi mbili rasmi za CAF. Morocco imetozwa faini ya Dola 200,000 kwa tabia isiyofaa ya wachezaji wa mpira uwanjani wakati wa fainali, huku faini ya Dola 100,000 ikitozwa kwa utovu wa nidhamu wa wachezaji wa Morocco na wafanyakazi wa kiufundi, ambao walivamia eneo la ukaguzi wa VAR na kuzuia kazi ya Mwamuzi. Aidha inaarifiwa kuwa, Morocco haitaandaa tena Fainali ya Kombe la Dunia la FIFA la 2030, kufuatia matukio wakati wa fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025. Mashindano hayo ya 2030 yanatarajiwa kuandaliwa kwa pamoja kati ya Uhispania, Ureno, na Morocco, huku Morocco wakiwa katika kinyang’anyiro cha kuandaa mechi ya fainali. Rafael Louzán, Rais wa Shirikisho la soka la Uhispania, alithibitisha kwamba Uhispania sasa itakuwa mwenyeji wa mechi ya fainali.
Mbali na hayo, Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC limeripoti kuwa, muungano wa wabunge 23 wasio na vyama vya siasa nchini Uingereza umesema utaliomba Shirikisho la Soka Duniani FIFA kutafakari suala la kuiondoa Marekani kwenye fainali za Kombe la Dunia la mwaka huu 2026. Mbali na ukosefu wa usalama ndani ya Marekani, ombi hili lisilo la kawaida linatokana na wasiwasi kuhusu vitendo vya hivi karibuni vya Rais Donald Trump kwenye jukwaa la kimataifa, ikiwa ni pamoja na kumteka nyara Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro na vitisho vikali vya Marekani dhidi ya nchi mbalimbali duniani. Glenn Tones, mtumiaji mashuhuri wa mtandao wa kijamii wa X aliandika hivi karibuni kwamba, nchi inayotishia amani ya dunia kila siku haipaswi kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia au Michezo ya Olimpiki. "Nilifuta tiketi zangu za Kombe la Dunia kwa sababu si salama kusafiri kwenda Marekani," Mohamed Safa, mkurugenzi mtendaji wa PVA Patriotic Vision, ambalo ni shirika lisilo la kiserikali linaloushauri Umoja wa Mataifa, ameviambia vyombo vya habari vya Mexico. Kiungo wa kati wa Ujerumani Leon Goretzka ambaye anakipiga katika kalumashuhuri ya Bayern Munich ya Ligi Kuu ya Kandanda ya Ujerumani (Bundesliga) amemshambulia Rais wa Marekani Donald Trump kwa kombora la kinaya akisema, "Trump ameweza kutufanya tujisikie sio tu kwamba ni Wajerumani, bali pia wazungu".

Baadhi ya wanasiasa wa Ujerumani wametishia kwamba timu ya taifa ya soka ya nchi hiyo inaweza kususia Kombe la Dunia la 2026. Malalamiko ya Ujerumani, ambayo yaliibuliwa na Jürgen Hardt, mwanachama wa Chama cha Kidemokrasia cha Kikristo na mshirika wa karibu wa Chansela Friedrich Merz, yanatokana na uchu wa Marekani wa kukitwaa kisiwa cha Greenland. Habari zaidi zinasema kuwa, mashabiki wa mpira wa miguu kutoka Ulaya, Afrika, Asia, na Amerika Kusini wanaogopa kusafiri katika mazingira ya sasa ya kisiasa yanayozidi kuwa mbaya na yenye uadui, huku baadhi ya nchi zikiwapiga marufuku raia wao kusafiri kwenda Marekani. Hoteli kadhaa huko Minneapolis na St. Paul nchini Marekani zimefungwa kutokana na wasiwasi kuhusu usalama wa watalii. Bodi ya Wakurugenzi ya Mile Lux Corporate Ventures imesema katika taarifa kuwa: "Tumeamua kufunga kwa muda hoteli zetu mbili huko St. Paul - InterContinental St. Paul Riverfront na DoubleTree St. Paul Downtown kutokana na wasiwasi mkubwa wa usalama." Kwa upande wake, mwanasiasa wa Uingereza George Galloway anasema: "Ni mwendawazimu tu ndiye atasafiri kwenda Marekani kwa ajili ya Kombe la Dunia la FIFA. Utakuwa na bahati mzuri kutoka nchini humo ukiwa hai. Hata kama wewe ni mzungu!" Siku chache zilizopita, Rais wa Shirikisho la Soka la Ujerumani (DFB), alisema wakati umeadia wa kujiondoa kwenye Kombe la Dunia la 2026 kutokana na hatua ya Rais wa Marekani Donald Trump, ya kutaka kutwaa kisiwa cha Greenland, ambacho kwa sasa kinasimamiwa na Denmark. Marekani ni mwenyeji wa mashindano ya mwaka huu ya Kombe la Dunia ikishirikiana na nchi za Canada na Mexico. Marekani itakuwa mwenyeji wa mechi 78 kati ya 104 za mashindano hayo. Huku muda wa mashindano hayo makubwa zaidi ya mpira wa miguu yatakayofanyika Juni 11 hadi Julai 19 ukizidi kujongea, ndivyo miito ya kuyasusia inazidi kutolewa. Oke Gottlich, rais wa klabu ya Bundesliga St Paul, na mmoja wa makamu wa rais 10 wa shirikisho la soka Ujerumani, alisema karibuni kuwa, wakati umefika wa "kufikiria kwa uzito na kujadili (suala) hili (la kususia Kombe la Dunia 2026)."
Kadhalika Rais wa zamani wa FIFA Sepp Blatter katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X, alimnukuu Mark Pieth - wakili wa Uswisi aliyebobea katika masuala ya uhalifu na mtaalamu wa kupambana na ufisadi, ambaye aliwataka mashabiki kususia Kombe la Dunia - na kuongeza, "Nadhani Mark Pieth yuko sahihi kuwa na mashaka na Kombe hili la Dunia."
Na Chama cha Soka cha China kimewapiga marufuku ya daima watu 73, akiwemo kocha mkuu wa zamani wa timu ya taifa Li Tie, sanjari na kuzipa adhabu klabu 13 za haiba, kutokana na upangaji wa matokeo na ufisadi. Chini ya utawala wa Rais Xi Jinping, msako mkali dhidi ya mafisadi umeenea katika soka la China katika miaka ya hivi karibuni, na kufichua uozo kwenye mchezo huo unaopendwa sana duniani. Miongoni mwao ni Chen Xuyuan, mwenyekiti wa zamani wa shirikisho la soka China CFA, ambaye tayari anatumikia kifungo cha maisha jela kwa kupokea rushwa ya dola milioni 11.
…………………TAMATI………….….