May 04, 2024 02:32 UTC
  • Afisa wa kijeshi wa Israel: Kuivamia Rafah si hakikisho la kuwakomboa mateka

Afisa wa zamani wa wizara ya vita ya utawala wa Kizayuni wa Israel amesema, uvamizi wa jeshi la utawala huo katika mji wa Rafah si hakikisho la kukombolewa na kurejeshwa mateka wake wanaoshikiliwa na makundi ya Wapalestina.

Amos Gileadi, ambaye ni mkurugenzi wa zamani wa sera na masuala ya kisiasa na kijeshi katika wizara ya vita ya Israel amebainisha hayo katika mahojiano na kituo cha redio cha Kizayuni cha FM 103 na kuongeza kwa kusema: "kuingia kwetu Rafah si hakikisho la kurejeshwa mateka".
 
Licha ya kuongezeka upinzani wa kimataifa, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa kuwa ataivamia kijeshi Rafah, ambayo sasa imekuwa makazi ya Wapalestina zaidi ya milioni moja na laki nne waliolazimika kuyahama makazi yao katika maeneo mengine ya Ukanda wa Ghaza.
Athari za mashambulio ya kinyama ya utawala wa Kizayuni Ghaza

Gileadi amesema: "iwapo tutaingia Rafah bila uratibu na Wamisri na Wamarekani, hatutapata suluhisho kwa upande wa kaskazini (kwenye mpaka wa Lebanon), na kutakuwa na vita vya muda mrefu ambavyo vitaenea Israel yote na kwa hiyo tutapoteza miungano yetu ya kimkakati”.

 
Redio ya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel iliripoti siku ya Alhamisi kwamba utawala huo unatafuta njia mbadala za uvamizi wake uliopangwa kufanywa dhidi ya mji wa Rafah, ulioko kwenye ncha ya kusini ya Ukanda wa Ghaza.
 
Afisa huyo wa zamani katika wizara ya vita ya utawala wa Kizayuni ameeleza hayo baada ya kituo cha binafsi cha habari cha Al-Qahera kunukuu duru za ngazi ya juu za Misri zikiripoti kwamba kuna "hatua nzuri" zilizopigwa katika mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana kati ya Israel na makundi ya Muqawama ya Palestina juu ya suala la kubadilishana mateka na kusitisha mapigano katika Ukanda wa Ghaza.../

 

Tags