May 04, 2024 02:30 UTC
  • Kashfa ya kutoweka raia 10,000 wa Palestina katika vita vya Gaza

Sambamba na kuendelea kupanuka maandamano ya wanafunzi wa Marekani na juhudi za Mahakama ya ICJ na ICC za kutoa waranti wa kukamatwa viongozi wa utawala wa kibaguzi wa Israel kutokana na jinai zao huko Gaza, Shirika la Haki za Binadamu la Euro-Mediterranean limetoa ripoti mpya na ya kutisha inayoweza kuzidisha hasira za wanafunzi hao na wakati huo huo kuongeza ushahidi mpya katika jinai zinazofanywa na utawala huo dhidi ya Wapalestina.

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Euro-Mediterranean limekusanya ushahidi wa kuaminika na taarifa za msingi zinazofichua sehemu iliyofichwa ya mauaji ya kutisha ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza. Ushahidi huo unaonyesha kwamba ndege za kivita za Israel zinarusha mabomu kwenye nyumba za makazi za Gaza ambayo yanaweza kutia joto kali na kuyeyusha miili ya watu.

Kwa hakika matokeo ya uchunguzi wa shirika hilo yanafichua ni kwa nini miili ya wakazi 10,000 wa Gaza ambao waliuawa wakati wa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika ukanda huo bado haijapatikana hadi sasa.

Shirika la Misaada kwa Watu wa Gaza limesema katika taarifa kwamba: "Makadirio yetu ni kwamba kuna zaidi ya watu 10,000 waliotoweka ambao wamesalia chini ya vifusi vya mamia ya majengo yaliyoharibiwa tangu kuanza uvamizi hadi leo. Makundi ya kitaalamu ya waokoaji hawajaweza kuipata miili hiyo hadi sasa. Idadi hii ya mashahidi haijasajiliwa katika nyaraka za hospitali wala ripoti za Wizara ya Afya. Kwa hiyo, idadi hiyo ni zaidi ya watu 44,000 waliotangaza rasmi." Mashambulizi ya makusudi ya Israeli kwa lengo la kusababisha uharibifu mkubwa katika maeneo ya makazi na kuua idadi kubwa ya watu huko Gaza, yameibua wasiwasi juu ya uwezekano wa utawala huo wa kigaidi kutumia "silaha za joto" au kwa jina jingine "mabomu ya ombwe" dhidi ya wanadamu.

Jinai ya Wazayuni dhidi ya Wapalestina

'Bomu la ombwe' au 'bomu la thermobaric' ni bomu lenye nguvu kubwa ya kusababisha mlipuko. Bomu hili hutumia kiwango kikubwa cha oksijeni iliyo pembeni yake, na hivyo kusababisha eneo ombwe lisilo na gesi hiyo. Kukosekana hewa ya oksijeni na kuundwa ombwe hilo husababisha mbano mkali wa hewa. Mabomu ya ombwe yameundwa kwa karibu asilimia 100 ya mafuta na hutegemea sana oksijeni iliyoko hewani kulipuka. Mabomu hayo yanaweza kurushwa kama kombora au kudondoshwa kutoka kwenye ndege za kivita.

Baada ya kupiga shabaha, mlipuko wa kwanza husababisha tanki la mafuta kufunguka na wingu kubwa la mlipuko kuenea mahala panapolengwa. Kisha, mlipuko wa pili huwasha wingu hilo na kusababisha mlipuko mkubwa sehemu hiyo. Baada ya kutokea mlipuko na wimbi la mshtuko, ombwe hudhihirika ambapo mchakato wa kunyonywa oksijeni hutokea katika eneo na hivyo kufyonza oksijeni kutoka kwenye mapafu ya wahanga na hatimaye kuwaua kinyama.

Hatua ya utawala haramu wa Israel ya kutumia silaha zilizopigwa marufuku kimataifa haihusishwi tu na kutumia kwake mabomu ya kuyeyusha maiti na kunyonga wahanga kwa kuwanyima hewa, wakiwemo watoto na wanawake wa Palestina, bali jeshi katili la utawala huo siku zote limekuwa likitumia aina mbalimbali za silaha na mabomu yenye uharibifu mkubwa dhidi ya raia hao wasio na hatia. Jambo hilo bila shaka linakiuka wazi sheria za kimataifa zinazowalinda raia na mali zao wakati wa vita.

Ushahidi na uchanguzi umethibitisha wazi kuwa jeshi la utawala huo wa kibaguzi limetumia mara kadhaa mabomu ya tani moja katika maeneo ya makazi ili kufikia malengo yake haramu. Pia limetumia mara nyingi mabomu ambayo huchoma vikali miili ya maelfu ya wahanga, kuwasababishia majeraha yanayopatwa na maambukizi yanayoenea kwa haraka na kisha kuwaua. Wizara ya Afya ya Gaza imepokea ripoti kutoka kwa hospitali, madaktari wa upasuaji na idara za watu waliochomeka miili kuhusu majeraha ya aina hiyo, ambayo yanaonyesha kuwa silaha zinazotumiwa na Wazayuni huyeyusha tabaka za kwanza la ngozi, ambayo ina jukumu la kulinda mwili dhidi ya maradhi ya vijidudu na kufikia tishu za ndani, na hii kuwa sababu kuu inayoongeza vifo vya wahanga wa mauaji hayo ya makusudi ya Wazayuni.

Uharibifu wa makusudi unaofanywa na Wazayuni katika makazi ya Wapalestina

Kwa hiyo, hakuna shaka kwamba rekodi ya utawala wa kigaidi wa Israel katika kutenda jinai za kutisha na ukiuka wa sheria za kimataifa na za kibinadamu, ni nyeusi sana na inapingana wazi na mikataba muhimu ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Mikataba ya Hague ya 1899 na 1907 pamoja na Mkataba wa Geneva wa 1949. Mikataba hiyo inapinga wazi matumizi ya mabomu ya joto katika maeneo ya makazi na kupiga marufuku kulengwa raia vitani. Ukiukaji wa makusudi wa mikataba hii umeifanya kadhia ya jinai za kivita za Israel na serikali ya mrengo wa kulia ya Benjamin Netanyahu kuwa kubwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Hivi sasa walimwengu wanasubiri kuona iwapo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC itawafungulia mashtaka wahusika wa jinai hizo za kivita huko Gaza au itaamua kukaa kimya na kufumbia macho jinai hizo kutokana na mashinikizo ya watawala wa Marekani.

Tags