Uingereza yaanza kuwashikilia wahamiaji wanaotarajiwa kupelekwa Rwanda
https://parstoday.ir/sw/news/world-i111298-uingereza_yaanza_kuwashikilia_wahamiaji_wanaotarajiwa_kupelekwa_rwanda
Mamlaka husika nchini Uingereza zimeanza kuwashikilia wahamiaji kama sehemu ya maandalizi ya kuwahamishia nchini Rwanda katika muda wa wiki 9 hadi 11 zijazo. Serikali ya London ilitangaza taarifa hiyo jana ikiashiria hatua muhimu katika mkakati wa uhamiaji unaotekelezwa na Waziri Mkuu Rishi Sunak.
(last modified 2024-05-02T04:01:35+00:00 )
May 02, 2024 04:01 UTC
  • Uingereza yaanza kuwashikilia wahamiaji wanaotarajiwa kupelekwa Rwanda

Mamlaka husika nchini Uingereza zimeanza kuwashikilia wahamiaji kama sehemu ya maandalizi ya kuwahamishia nchini Rwanda katika muda wa wiki 9 hadi 11 zijazo. Serikali ya London ilitangaza taarifa hiyo jana ikiashiria hatua muhimu katika mkakati wa uhamiaji unaotekelezwa na Waziri Mkuu Rishi Sunak.

Maafisa wa idara ya uhamiaji ya Uingereza katika mpango huo tajwa wameonakana wakiingia katika nyumba mbalimbali na kuwatoa watu wakiwa na pingu mikononi. 

Serikali ya Uingereza imeeleza kuwa timu za utendaji ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani zimekuwa zikifanya kazi kwa kasi kuwaweka kizuizini kwa usalama na haraka watu walioorodheshwa katika mkakati huo wa Waziri Mkuu Sunak ili kupatiwa hifadhi huko Rwanda. 

Ripoti kutoka taasisi ya kujitolea ya kuhudumia wakimbizi ya Care4Calais imethibitisha kuwa zoezi la kuwakamata na kuwashikilia raia hao wanaotazamiwa kupelekwa Rwanda lilianza Jumatatu.  

Wakati huo huo picha zilizorushwa jana katika mitandao ya kijamii na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza zimewaonyesha raia hao wakiwa chini ya udhibiti wa maafisa husika wa uhamiaji. 

James Cleverly Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza jana alieleza kuwa timu zao za kutekeleza sheria zilizojitolea zinafanya kazi kwa bidii ili kuwakamata mara moja wale wasio na hadhi halali ili waweze kuharakisha mchakato wa kuanza safari za ndege kuekelea Rwanda.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza, James Cleverly