Mar 12, 2024 06:14 UTC
  • Mohamed Elneny
    Mohamed Elneny

Nyota wa timu ya taifa ya Misri, Mohamed Elneny, na mchezaji wa timu ya soka ya Uingereza ya Arsenal, amezindua chumba cha kwanza cha Swala kwa ajili ya wachezaji wa Kiislamu kwenye Uwanja wa Emirates uliopo katika mji mkuu wa Uingereza, London, suala litakalowawezesha kusali na kuabudu katika eneo hilo katika mwezi wa huu wa Ramadhani ulioanza jana Jumatatu, nchini Uingereza.

Mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Misri alionekana akiwa ameshika mkasi na kukata utepe wa kufungua chumba cha ibada ya Swala akiushukuru uongozi na timu ya Arsenal.

Elneny amesema kupitia akaunti yake kwenye jukwaa la (X) kwamba: "Kuwapo nafasi hii ya kutafakari na kufanya ibada kutabadili maisha ya wachezaji wa Arsenal katika siku zijazo.

Ninawashukuru sana maafisa na wale wote waliohusika katika kufanikisha suala hili."

Mohamed Elneny ni maarufu kwa misimamo yake ya kutetea na kuunga mkono masuala ya Umma wa Kiislamu, na msimamo wake wa hivi sasa ni kutangaza mshikamano wake na watu wa Ukanda wa Gaza dhidi ya uvamizi wa Israel.

Uwanja wa Emirates, ulioko Holloway, kaskazini mwa London, Uingereza, ndio uwanja mkuu wa timu ya Arsenal, na ulifunguliwa Julai 2006.

Tags