May 02, 2024 03:25 UTC
  • Colombia yaamua kuvunja uhusiano na Israel kwa sababu ya mauaji ya kimbari ya Ghaza

Colombia imeamua kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na vita vya kinyama na mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na utawala huo haramu dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza.

Rais Gustavo Petro, ambaye ni mkosoaji mkubwa wa mashambulizi ya kikatili yanayofanywa na Israel huko Ghaza, alitangaza uamuzi huo jana alipohutubia maandamano ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (May Day) katika mji mkuu wa nchi hiyo Bogota.
 
Akitangaza uamuzi huo, Rais wa Colombia alisema: "na sisi hapa mbele yenu, serikali ya mabadiliko, rais wa jamhuri anataarifu kwamba kesho (Alkhamisi) uhusiano wa kidiplomasia" na utawala wa Israel "utakatwa".
 
Amesisitiza kuwa serikali ya Bogota inachukua uamuzi huo kwa sababu ya utawala wa Kizayuni kuwa na rais muhusika wa mauaji ya kimbari.
Rais Gustavo Petro

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Petro ameashiria maandamano ya umma yanayoendelea kufanyika duniani kote kupinga vita dhidi ya Ghaza tangu vilipoanzishwa na utawala wa Kizayuni Oktoba 7, 2023 na kusema, anaamini wanadamu wote kwa mamilioni wanaomiminika mitaani wanakubaliana na msimamo wa Colombia na Colombia nayo inakubaliana nao na akafafanua kwa kusema: "haiwezi kuwa, hawawezi kurudi kwenye zama za mauaji ya kimbari, ya kuangamizwa watu wote mbele ya macho yetu, mbele ya kimya chetu. Ikiwa Palestina itakufa, ubinadamu utakufa na hatutaiacha ife kama ambavyo hatutauacha ubinadamu ufe."

Mnamo mwezi Oktoba 2023 pia, Rais wa Columbia alimshambulia vikali waziri wa vita wa utawala wa Kizayuni Yoav Gallant kwa kutumia lugha dhidi ya watu wa Gaza ambayo alisema ni sawa na waliyoitumia Wanazi kuhusu Wayahudi. Utawala wa Kizayuni uliamua "kusimamisha usafirishaji wa vifaa vya masuala ya usalama" kwa nchi hiyo ya Amerika ya Kusini.

Mwezi Februari, Rais Petro alisimamisha ununuzi wa silaha za Israel baada ya shambulio la kinyama la jeshi la utawala huo ghasibu dhidi ya Wapalestina wa Ghaza, waliokuwa wamekusanyika kupokea msaada wa kibinadamu, akisema shambulio hilo "linaitwa mauaji ya kimbari na linakumbusha mauaji ya Holocaust."

Wapalestina wasiopungua 34,568 wengi wao wakiwa wanawake, watoto na vijana wameshauawa shahidi hadi sasa katika vita vya kinyama vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni tarehe 7 Oktoba kufuatia operesheni ya ulipizaji kisasi ya Kimbunga cha Al-Aqsa iliyotekelezwa na makundi ya Muqawama ya Ghaza.../

Tags