Polisi wa Marekani watumia mabavu kuwatawanya wanafunzi wanaounga mkono Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/world-i111348-polisi_wa_marekani_watumia_mabavu_kuwatawanya_wanafunzi_wanaounga_mkono_palestina
Polisi wa kuzima ghasia nchini Marekani wameibomoa kambi ya wanafunzi wanaoandamana kwa amani kuunga mkono Palestina katika Chuo Kikuu cha California huko Los Angeles, siku moja baada ya wanafunzi hao kushambuliwa na wafuasi wanaounga mkono utawala haramu wa Israel.
(last modified 2024-05-03T07:08:53+00:00 )
May 03, 2024 07:08 UTC
  • Polisi wa Marekani watumia mabavu kuwatawanya wanafunzi wanaounga mkono Palestina

Polisi wa kuzima ghasia nchini Marekani wameibomoa kambi ya wanafunzi wanaoandamana kwa amani kuunga mkono Palestina katika Chuo Kikuu cha California huko Los Angeles, siku moja baada ya wanafunzi hao kushambuliwa na wafuasi wanaounga mkono utawala haramu wa Israel.

Takriban waandamanaji 200 wanaoiunga mkono Palestina walikamatwa wakati wa vurumai hiyo Alhamisi. Kulingana na makadirio ya kituo cha runinga cha KABC-TV, waandamanaji 300 hadi 500 walivamiwa ndani ya kambi hiyo, wakati takriban 2,000 zaidi walikuwa wamekusanyika nje ya vizuizi kuwaunga mkono wenzao.

Polisi wa Marekani wamewakamata takriban wanafunzi 2,200 wakati wa maandamano ya wafuasi wa Palestina katika vyuo vikuu kote nchini katika wiki za hivi karibuni.

Wanafunzi wa matabaka mbalimbali katika vyuo vikuu vya Marekani wameonyesha mshikamano na kuwaunga mkono pakubwa watu wa Gaza, na wakati huo huo kupinga vikali sera za serikali ya Biden za kuuhami kwa pande zote utawala haramu wa Israel. Mnamo Aprili 17, vuguvugu la nchi nzima kwa jina la "Solidarity Movement with Gaza" lilianza kufanya maandamano ya kuiunga mkono Palestina kutokea Chuo Kikuu cha Columbia mjini New York tangu kuanza kwa maandamano ya kupinga vita vya Israel huko Gaza, ambavyo vimepelekea kuuliwa shahidi makumi ya maelfu ya watu, ambapo sasa maandamano hayo yameenea katika vyuo vikuu vingine huko Marekani.

Wanafunzi hao wanataka utawala wa Kizayuni wa Israel usitishe mara moja  vita vya mauaji ya halaiki dhidi ya Gaza. Aidha wanataka vyuo vikuu Marekani visitishe uhusiano wowote ule na utawala haramu wa Israel.