Kuuawa na kujeruhiwa makumi ya Waislamu Msikitini nchini Pakistan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i93554-kuuawa_na_kujeruhiwa_makumi_ya_waislamu_msikitini_nchini_pakistan
Watu wasiopungua mia moja wameuawa na kujeruhiwa katika mripuko mkubwa uliotokea ndani ya Msikiti kwenye mji wa Peshawar nchini Pakistan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 01, 2023 10:47 UTC
  • Kuuawa na kujeruhiwa makumi ya Waislamu Msikitini nchini Pakistan

Watu wasiopungua mia moja wameuawa na kujeruhiwa katika mripuko mkubwa uliotokea ndani ya Msikiti kwenye mji wa Peshawar nchini Pakistan.

Televisheni ya al Jazeera ya Qatar imenukuu duru za usalama za Pakistan zikisema kuwa, watu wasiopungua 56 wameuawa na makumi ya wengine wamejeruhiwa katika mripuko huo ulitokea wakati wa Sala ya Adhuburi siku ya Jumatatu, katika mji huo wa Peshawar wa kaskazini maghribi mwa Pakistan. Duru za hospitali na usalama zimesema kuwa, kuna uwezekano wa kuongezeka idadi ya watu waliouawa kutokana na hali za baadhi ya majeruhi kuwa mahututi. Inaonekana genge la kitaidi la "Tehrik-i-Taliban Pakistan" ndilo lililohusika na jinai hiyo kwani limekuwa likitoa vitisho mtawalia dhidi ya serikali na jeshi la Pakistan. Lakini pia kutokana na kwamba, shambulio hilo limetokea Msikitini na idadi kubwa ya Waislamu wameuawa wakiwa ndani ya Sala, inaonekana si genge hilo pekee lililohusika na shambulio hilo. Alaakullihaal, mripuko wa Peshawar unaonesha kuwa, mashambulio ya kigaidi yameongezeka katika maeneo tofauti ya Pakistan.

Mashambulizi hayo yana malengo tofauti. Kwanza ni kwamba makundi ya kigaidi yanajaribu kuonesha nguvu zao mbele ya jeshi la Pakistan ambalo linahesabiwa kuwa moja ya majeshi yenye nguvu zaidi katika eneo hili. Pili ni kwamba magenge hayo ya kigaidi yanalenga Misikiti ili kuchochea vita vya kidini, kikabila na kimadhehebu nchini Pakistan. Molavi Moflih, mtaalamu wa masuala ya kisiasa na kidini anasema:

Magaidi wanataka kuzusha vita vya kikabila na kidini nchini Pakistan. Magaidi hao wanaonesha nguvu zao mbele ya jeshi la Pakistan na kujaribu kulidhoofisha jeshi hilo. Wanafanya mashambulio ya umwagaji wa damu hasa Misikitini ili kuonesha kuwa bado wana nguvu na hii ni katika hali ambayo kuua Waislamu tena ndani ya Nyumba ya Allah yaani Msikitini, kwa hali yoyote iwayo, ni kitendo kisicho na chembe ya ubindamu na ni kwa manufaa ya maadui wa Uislamu na ni madhara kwa Uislamu na Waislamu.

Takwimu zinaonesha kuwa, mwaka 2022, kulisajiliwa mashambulio 500 ya kigaidi nchini Pakistan na sehemu kubwa ya mashambulio hayo yalifanywa na kundi hilo la "Tehrik-i-Taliban Pakistan." Kwa kuzingatia kuwa hivi sasa kuna miungano ya makundi ya kigaidi, kumejitokeza wasiwasi kati ya wananchi wa Pakistan kwamba magaidi wameamua kutumia mbinu zote za kijinai kufanya mauaji na vitendo vya kigaidi dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo. Amma kwa upande wa malengo mengine ni kwamba shabaha nyingine za magaidi hao ni kuiweka chini ya mashinikizo serikali na jeshi la Pakistan ili wakubali kufanya mazungumzo na magenge hayo ya kigaidi. Kundi la "Tehrik-i-Taliban Pakistan" limejitoa kwenye mazungumzo na serikali ya nchi hiyo na hivi sasa linaiweka serikali ya Pakistan chini ya mashinikizo kwa kutumia mbinu tofauti ili kuishinikiza serikali hiyo ikubali kufanya mazungumzo na genge hilo. 

Alaakullihaal, mripuko mkubwa uliotokea Msikitini huko Peshawar, kaskazini magharibi mwa Pakistan unaonesha kuwa, magenge ya kigaidi kama Sepahe Sahabe na Lashkar-e-Jhangvi pamoja na "Tehrik-i-Taliban Pakistan" yameamua kutorudi nyuma katika jinai zao za kuua Waislamu wasio na hatia. Msingi mkuu wa kifikra wa magenge hayo ni Uwahabi na ya ukufurshaji na vitendo vyao vinauhudumia moja kwa moja utawala wa Kizayuni wa Israel na madola ya kibeberu. Hivyo wanachokitarajia wananchi Waislamu wa Pakistan hivi sasa ni kuona maulamaa wa nchi hiyo wakijitokeza na kulaani jinai hizo ikiwemo hii ya ndani ya Msitiki huko Peshawar ili kuyavunja nguvu magenge hayo ya kigaidi. Ni wazi kwamba kuendelea kukaa kimya maulamaa hao kutakuwa ni aina fulani ya kuridhishwa kwao na vitendo hivyo vya kigaidi na ni katika kuyapandisha kichwa magenge hayo, cha kufanya jinai kubwa zaidi dhidi ya Waislamu wa Pakistan.