Nchi za Amerika ya Latini zalaani ujenzi wa vitongoji haramu
(last modified Sat, 18 Feb 2023 09:53:55 GMT )
Feb 18, 2023 09:53 UTC
  • Nchi za Amerika ya Latini zalaani ujenzi wa vitongoji haramu

Kundi la nchi za Amerika ya Latini limelaani na kukosoa vikali uamuzi wa serikali ya Israel yenye misimamo ya kufurutu ada ya Benjamin Netanyahu wa kuidhinisha ujenzi wa vitongoji vipya tisa katika ardhi za Wapalestina za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Brazil iliyotiwa saini pia na nchi za Argentina, Chile, na Mexico imesema nchi hizo za Amerika ya Latini zinatiwa wasiwasi na tangazo la Israel la Februari 12, kwamba itaruhusu ujenzi huo wa nyumba 9, kama sehemu ya ujenzi wa nyumba 10,000 katika eneo linalikaliwa kwa mabavu la Ukingo wa Magharibi.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, uchukuaji uamuzi huo wa upande mmoja wa Israel wa kujenga vitongoji zaidi vya walowezi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu tangu mwaka 1967,  si halali na ni kinyume cha kisheria, na ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Kwa muda mrefu sasa, aghalabu ya nchi za Amerikali ya Latini zimekuwa zikitangaza wazi wazi uungaji mkono wao kwa wananchi madhulumu wa Palestina, sambamba na kupinga sera kandamizi na jinai za Israel mkabala wa Wapalestina.

Ukuta wa kibaguzi eneo la Ukingo wa Magharibi

Mwaka 2020, Wabunge wa baadhi ya nchi za Amerika ya Latini walitaka kutungwe sheria za kuususia na kuuwekea vikwazo utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na mpango wa utawala huo ghasibu wa kutaka kupora ardhi zaidi za Wapalestina za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Kadhalika dunia nzima inapinga njama za Wazayuni za kutaka kuteka ardhi zaidi za Wapalestina. Hivi sasa kuna rasimu ya azimio jipya la Umoja wa Mataifa ambayo inautaka utawala ghasibu wa Israel kukomesha haraka iwezekanavyo shughuli za upanuzi wa vitongoji vya walowezi wake katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.