Kampuni za silaha za US zashtakiwa kwa jinai za kivita Yemen
Mashirika ya kuzalisha silaha ya Marekani yamefunguliwa mashitaka yakituhumiwa kusaidia na kuwa 'mshiriki' wa jinai za kivita nchini Yemen.
Faili hilo dhidi ya kampuni za silaha za Marekani za Raytheon, Lockheed Martin na General Dynamics limewasilishwa na raia saba wa Yemen mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Washington D.C.
Aidha faili hilo limewajumuisha Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia, Mohammad Bin Salman na mtawala wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Mohamed Bin Zayed Al-Nahyan, wakituhumiwa kuhusika kikamilifu na kuendelea hali mbaya ya kibinadamu huko Yemen.
Kadhalika Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken na Mkuu wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon), Lloyd Austin wameshtakiwa kwenye kesi hiyo ya kuhusika na jinai za kivita nchini Yemen.
Faili lililowasilishwa mahakamani na raia saba wa Yemen kwa niaba ya Wayemen wote linasema zaidi ya watu 25,000 wakiwemo watoto elfu 11 wa Yemen wameuawa tangu kuanza kwa mashambulizi ya muungano vamizi unaoongozwa Saudi Arabia mwaka 2015.

Wananchi wa Yemen wamekuwa wakisisitiza pia kwamba, Umoja wa Mataifa ni mshirika wa jinai za muungano vamizi huko Yemen unaoongozwa na Saudi Arabia.
Mapema mwaka huu, wananchi wa Yemen walifanya maandamano makubwa katika mikoa mbalimbali kulaani uvamizi wa muungano wa Saudia na Marekani dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu na kuendelea kuzingirwa kila upande nchi yao pamoja na vitendo mbalimbali vya kuchochea vita vinavyofanya na madola vamizi.