Mar 11, 2023 11:45 UTC
  • Kuvunjwa rasmi mpango wa INSTEX; nembo ya kukiukwa ahadi za Ulaya mkabala wa utekelezaji wa JCPOA

Troika ya Ulaya inayoundwa na Ujerumani, Ufaransa na Uingereza juzi Alhamisi ilitangaza katika taarifa yake kuwa imesitisha mfumo kwa jina la mpango wa mabadilishano ya kifedha na kibiashara "INSTEX" uliouanzisha mwaka 2019 kwa ajili ya kulinda biashara na Iran mkabala wa vikwazo vya Marekani.

Kama zilivyokiri nchi hizo, ni muamala mmoja tu wa kibiashara uliotekelezwa kupitia mfumo huo. Miezi 14 baada ya kuasisiwa yaani mwezi Machi mwaka 2020; mfumo wa INSTEX ulitekeleza muamala wa kwanza na wa pekee wa kibiashara kati yake na Iran kuhusu vifaa vya tiba.  

Nchi hizo zimeeleza katika taarifa yao ya pamoja kwamba, uamuzi wa kuuvunja mfumo wa INSTEX umechukuliwa kwa misingi ya masuala ya kibiashara na mengine binafsi. Mfumo wa INSTEX ulizinduliwa mwezi Januari 2019 yaani karibu miaka miwili baada ya Marekani kujitoa kwa upande mmoja katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA. 

Mapatano ya nyuklia ya JCPOA 

Pamoja na kuwa nchi za Ulaya zilikuwa zikidai kuwa zimeasisi mfumo huo kwa ajili ya kukabiliana na vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, lakini viongozi wa ngazi ya juu wa nchi hiyo mara kadhaa walikiri katika matamshi na maoni yao kuwa mfumo wa INSTEX ni hatua ya kinembo tu kwa kuzingatia kuwa makampuni binafsi hayawezi kulazimishwa kufanya kazi na nchi fulani.  

Licha ya kuwa pande  za Ulaya  zimejaribu hivi sasa kuinyoshea Iran kidole cha lawama kwa kusambaratisha INSTEX, lakini ukweli wa mambo ni kuwa kwa kuzingatia matakwa muhimu na ya msingi ya Iran kwa ajili ya kutekelezwa mfumo huu tajwa ili kufanikisha biashara kati yake na nchi za Ulaya ili kupunguza athari hasi za vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi yake lakini ni pande hizo hizo za Ulaya ndizo zimeshindwa kuutekeleza mfumo huo;  kwani makampuni, taasisi na benki za Ulaya hazikuwahi kushiriki kivitendo katika shughuli za kifedha na kibiashara na Iran kwa kuhofia kuadhibiwa na Washington.  

Ni dhahir shahir kuwa moja ya sababu kuu za kushindwa kufanya kazi mfumo wa INSTEX ni kusitasita kwa benki za Ulaya katika kufanya miamala inayohusiana na Iran kwa kuogopa kuwekewa vikwazo na Marekani.

Nassir Kana'ani Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amegusia kuhusu mfumo wa INSTEX na kusema: "Ijapokuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijawahi kuegemea kwa mfumo huu, lakini kwa nia njema kabisa haikusita kutoa ushirikiano wa iana yoyote kwa ajili ya kufanikisha mpango huo." 

Nassir Kana'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran  

Kana'ani amezituhumu serikali za Ulaya kwa kutotekeleza kivitendo na kufanikisha mfumo wa INSTEX na kubainisha kuwa: nchi za Ulaya hazikutekeleza hatua za lazima na za dharura za kuhuisha mfumo huo katika kalibu ya utekelezaji wa ahadi na majukumu yao kwa mujibu wa mapatano ya JCPOA. 

Wakati huo huo, Troika ya Ulaya imedai katika taarifa yake kuwa wabia 10 wa INSTEX yaani Ubelgiji, Ujerumani, Finland, Denmark, Ufaransa, Uholanzi, Norway, Uhispania, Sweden na Uingereza zimefikia natija hii kuwa, hakuna sababu ya kuendelea kufanya kazi na INSTEX baada ya Iran kukataa kufanya kazi na mfumo huo. 

Pande za Ulaya zinadai kuwa kutokana na sababu za kisiasa, Iran imezuia INSTEX kufanya kazi kwa kuzingatia ajenda yake. Katika taarifa hii, inadaiwa kuwa Iran imetoa tu ruhusa kwa muamala mmoja na kisha kuzuia miamala mingine.

Hii ni katika hali ambayo Tehran imedhihirisha msimamo wake kuhusu INSTEX baada ya kutokuwa na manufaa na kusita nchi za Ulaya kufanya miamala ya kibiashara na kifedha na Tehran. Pamoja na kuwa Iran ilitaraji kwamba baadhi ya hatua za Ulaya na hasa INSTEX zingetekelezwa ipasavyo hata hivyo pande hizo zimezembea waziwazi katika uwanja huo.

Kwa utaratibu huo, Iran ina shaka kuhusu uwezo au nia ya upande wa Ulaya ya kuyalinda mapatano ya JCPOA; na ndio maana iliamua hatua kwa hatua kupunguza majukumu yake ndani ya JCPOA.

Kimsingi ni kuwa licha ya kufanyika mazungumzo kwa miaka kadhaa huko Vienna na kuwa tayari kwa ajili ya kurejea katika mapatano ya JCPOA lakini pande za Ulaya hazitoi mashinikizo yoyote kwa Marekani. Washington pia licha ya madai yake ya huko nyuma ya serikali ya Biden kuhusu kurejea katika mapatano ya JCPOA hivi sasa imeshikilia msimamo huu kwamba mazungumzo kuhusu JCPOA si katika kipaumbele chake. Msimamo huu wa serikali ya Biden umekosolewa na Russia ambayo ni mwanachama wa kundi la 4+1.  

Mikhail Ulyanov Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika taasisi za kimataifa zenye makao yake mjini Vienna Austria amekosoa hatua ya Marekani na Ulaya ya kukwamisha kurejea kwenye mapatano ya JCPOA na kusema: Marekani haitarejea haraka katika meza ya mazungumzo." 

Mikhail Ulyanov 

Tags