Iran yatangaza orodha ya waliodhinishwa kugombea urais Juni 28
(last modified Mon, 10 Jun 2024 03:23:45 GMT )
Jun 10, 2024 03:23 UTC
  • Iran yatangaza orodha ya waliodhinishwa kugombea urais Juni 28

Makao Makuu ya Uchaguzi katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran yametangaza orodha ya mwisho ya viongozi waliodhinishwa kugombea uchaguzi wa mapema wa duru ya 14 ya urais wa Jamhuri ya Kiislamu.

Mohsen Eslami, Msemaji wa Makao Makuu ya Uchaguzi ya Iran amesema shakhsia sita ndio waliodhinishwa na Baraza la Kulinda Katiba la Iran lenye wanachama 12, kuwania uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika Juni 28 hapa nchini.

Waliodhinishwa ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Sheria wa Iran, Mostafa Pourmohammadi, Waziri wa zamani wa Afya, Massoud Pezeshkian, na Amirhossein Ghazizadeh-Hashemi, Mkuu wa Wakfu wa Masuala ya Mashahidi na Maveterani.

Wengine waliopasishwa kugombea nafasi hiyo iliyobaki wazi baada ya kufa shahidi Rais Sayyid Ebrahim Raisi katika ajali ya helikopta Mei 19 ni Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge), Mohammad Baqer Qalibaf, Meya wa jiji la Tehran, Alireza Zakani, na Saeed Jalili, mjumbe mkuu wa zamani wa mazungumzo ya nyuklia ya Iran.

Shahidi Rais Sayyid Ebrahim Raisi

Baadhi ya shakhsia wakubwa waliotemwa kwenye mchujo wa Baraza la Kulinda Katiba la Iran ni pamoja na Mahmoud Ahmadinejad, rais wa zamani wa Iran, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran, Es’haq Jahangiri na Mbunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Zohreh Elahian ambaye alikuwa mwanamke wa kwanza kujiandikisha kugombea uchaguzi wa rais wa mwaka huu 2024.

 Kampeni za uchaguzi zinatazamiwa kuanza wakati wowote tokea sasa, na zitaendelea hadi Juni 26, siku mbili kabla ya kufanyika uchaguzi.