Onyo dhidi ya wapinzani wa mfumo wa kifalme nchini Uingereza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i97108-onyo_dhidi_ya_wapinzani_wa_mfumo_wa_kifalme_nchini_uingereza
Kufuatia maandamano ya maelfu ya watu wanaoipinga familia ya kifalme ya Uingereza katika mji wa London, mbunge mmoja wa ngazi ya juu wa chama tawala cha kihafidhina cha nchi hiyo, ametoa matamshi yenye utata, akitaka wapinzani hao wafukuzwe nchini ikiwa hawawezi kumkubali mfalme wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 08, 2023 03:04 UTC

Kufuatia maandamano ya maelfu ya watu wanaoipinga familia ya kifalme ya Uingereza katika mji wa London, mbunge mmoja wa ngazi ya juu wa chama tawala cha kihafidhina cha nchi hiyo, ametoa matamshi yenye utata, akitaka wapinzani hao wafukuzwe nchini ikiwa hawawezi kumkubali mfalme wa nchi hiyo.

Lee Anderson, naibu kiongozi wa chama tawala cha kihafidhina, ametoa matamshi hayo yenye utata kupitia ujumbe alioandika katika mtandao wa twitter kufuatia kukamatwa mjini London kwa waandamanaji wa kundi la Republican ambao wanapinga utawala wa kifalme wa Uingereza, katika mkesha wa sherehe za kutawazwa Charles III kama mfalme mpya wa Uingereza. Katika matamshi yake ya kejeli na udhalilishaji dhidi ya nara za wapinzani Anderson amezitaja nara hizo kuwa za kipuuzi na kuhoji: "Yeye si mfalme wangu?! Ikiwa hutaki kuishi katika nchi ambayo kuna utawala wa kifalme, suluhisho sio kupiga nara zako za kijinga, bali suluhisho ni kuhama." Pia ameunga mkono ukandamizaji wa polisi dhidi ya waandamanaji waliokuwa wamebeba mabango yenye kauli mbiu inayosema "Yeye si mfalme wangu" karibu na kasri ya Buckingham. Hata kama matamshi hayo yenye utata yamekasolewa kwenye mitandao ya kijamii na kutajwa kuwa "yasiyo ya kidemokrasia", lakini baadhi ya watu wameunga mkono msimamo wake huo.

Lee Anderson

Msimamo mkali wa kiongozi huyu mkuu wa chama cha kihafidhina kuhusu ulazima wa kufukuzwa wapinzani wa mfumo wa kifalme nchini Uingereza unaonyesha hali ya serikali ya Uingereza kutoheshimu demokrasia na kutovumilia maoni ya wapinzani nchini. Katika hali ambayo wapinzani wa mfumo wa ufalme wametoa maoni yao kupitia maandamano ya amani, hatua ya ukadamizaji iliyochukuliwa dhidi yao inathibitisha wazi kuwa utawala wa Uingereza huwa hauvumilii upinzani hata wa kiwango cha chini kabisa, linapokuja suala la kupingwa mfumo wa kisiasa wa nchi hiyo, hasa utawala wa kifalme.

Kuhusiana na hilo, polisi wa Uingereza walimtia mbaroni Graham Smith, mkuu wa kundi la Republican linalopinga mfumo wa ufalme pamoja na watu wengine kadhaa waliokuwa wanafanya maandamano karibu na eneo la kutawazwa Mfalme Charles, kwa madai ya kusababisha fujo na kutatiza utulivu wa umma. Wafungwa kadhaa walisema katika mahojiano na Iranpress kwamba polisi wa Uingereza waliwapokonya maandishi, kuwafunga pingu na kuwatia mbaroni kwa kuandika nara za kupinga ufalme na kukosoa ukiukaji wa demokrasia kwenye mashati yao.

Wakati huo huo, sherehe za kutawazwa Charles III zimefanyika huku miito ya kutaka ufalme wa Uingereza usitishwe ikiongezeka kila siku. Kuchakaa kwa mfumo wa kifalme katika nchi nyingi za dunia na kuungwa mkono mfumo wa jamhuri ambapo viongozi waandamizi wa serikali na mfumo wa nchi huchaguliwa kwa kura za wananchi pia kumechangia ongezeko la matakwa ya kuachana na mfumo wa kifalme nchini Uingereza.

Kundi la Rebuplican ambalo lina maelfu ya wanachama na makumi ya maelfu ya mashabiki, huku likipinga madai kwamba mfumo wa kifalme wa nchi hiyo unawavutia watalii, linasisitiza kuwa mfumo huo ni ukumbusho wa dhuluma ambayo wafalme wa Uingereza waliifanya dhidi ya kamii ya mwanadamu katika karne zilizopita. Kundi hilo linataka kufanyika kura ya maoni juu ya mustakabali wa utawala wa kifalme huko Uingereza. Wakati huo huo, ushindi wa chama cha Republican cha Sinn Fein katika uchaguzi uliofanyika huko Ireland Kaskazini, kwa uchache unaonyesha kwamba, wengi wa wakazi wa eneo hilo, ambao ni Wakatoliki, wanapinga mfumo wa ufalme wa Uingereza. Hii ni katika hali ambayo Waprotestanti wa eneo hilo ambao ni waungaji mkono wa mfumo wa ufalme, wanapinga vikali kuvunjwa kwake.

Mfalme Charles III baada ya kuvikwa taji la ufalme

Licha ya historia ndefu ya utawala wa kifalme nchini Uingereza, upinzani dhidi yake umeongezeka katika miongo ya hivi karibuni kwa sababu mbalimbali. Miongoni mwa sababu hizo ni kashfa za maadili na talaka nyingi katika familia ya kifalme, gharama kubwa za kuendesha familia ya kifalme, tokea kwenye ndoa hadi sherehe za mazishi na uvikaji taji pamoja na mishahara mikubwa ya familia hiyo kutoka kwenye hazina ya serikali.

Suala jingine muhimu linalohusiana na familia ya kifalme ya Uingereza ni kuwepo ubaguzi, hitilafu na mivutano mikubwa ndani ya familia hiyo. Kwa mfano, "Meghan Markle", mke wa Prince Harry, mjukuu wa Malkia Elizabeth, alizungumzia wazi uwepo wa ubaguzi wa rangi katika familia hiyo katika mahojiano aliyofanyiwa mnamo Machi 2020. Rangi ya ngozi ya Meghan na kutoka kwake katika familia ya kawaida hayakuwa mambo yaliyokubaliwa kirahisi na wakaazi wa kasri ya Buckingham. Ni wazi kuwa kuendelea mfumo wa kifalme nchini Uingereza kunaongeza gharama kubwa katika bajeti ya nchi. Bila shaka gharama ya kutawazwa Mfalme Charles III wa Uingereza ilidhaminiwa na serikali kutoka kwenye mfuko wa walipa kodi wa nchi hiyo. Wataalamu wa mambo wanakadiria kuwa takriban euro milioni 57 hadi 113 zilitumika kwa ajili ya hafla hiyo.