May 10, 2024 09:54 UTC
  • Ripoti yafichua: Chama tawala Kenya kiliazimia kuua Azimio la Umoja-One Kenya

Vyombo vya habari vya Kenya vimefichua kuwa, mabadiliko ya siri yaliyotayarishiwa miswada ya kufanikisha utekelezaji wa ripoti ya Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (NADCO) iliyowasilishwa majuzi katika Seneti ya nchi hiyo yamefuchua njama ya kuvunja chama cha Azimio la Umoja-One Kenya kinachoongozwa na Raila Odinga.

Imegundulika kuwa kulikuwa na njama iliyopangwa na mrengo wa chama tawala, Kenya Kwanza, unaoongozwa na Rais William Ruto, kufanya mabadiliko katika Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa ya 2024 ili kufutilia mbali vyama vya miungano.

Hatua hiyo ingeua kabisa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya unaoongozwa na Raila Odinga, ambao unatambuliwa kama chama cha kisiasa na muungano wa vyama, kwa wakati mmoja.

Njama hiyo ilitibuliwa wiki hii na Kiongozi wa Wachache katika Seneti ya Kenya, Stewart Madzayo, aliyewasilisha malalamishi kwa Spika Amason Kingi ambaye aliamuru kuondolewa muswada huo baada ya kuwasilishwa na Kiongozi wa Wengi, Aaron Cheruiyot.

Bw Madzayo, ambaye ni Seneta wa Kilifi, amesema hatua ya mrengo wa Kenya Kwanza kupendekeza kuwa Sheria ya Marekebisho ya Vyama vya Kisiasa ya 2022 ifanyiwe marekebisho kwa kuondoa kiashirio, “chama cha muungano wa vyama vya kisiasa,” ingeua kabisa Azimio la Umoja-One Kenya “pamoja na haki na manufaa yote inayopata bungeni na katika sheria.

Raila na Ruto

Madzayo, ambaye ni mwanasheria na jaji mstaafu, ameongeza kuwa: "Azimio ndicho chama cha muungano cha kipekee nchini na ukiondoa kiashirio hicho, basi unalenga Azimio. Iwapo muswada huo ungepitishwa ulivyokuwa, Azimio haingekuwepo tena. Tungerejesha taifa hili katika utawala wa chama kimoja."

“Inasikitisha kuwa ukora kama huu unaweza kutokea katika kizazi cha sasa. Watu hawafai kuendesha njama kama hii ikiwa kweli tunaheshimu na kuipa uzito demokrasia yetu,” amesema Seneta Madzayo. 

Tags