Apr 26, 2024 03:09 UTC
  • Marekani yashadidisha ukandamizaji dhidi ya wapinzani wa utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wa Palestina

Marekani ndiyo muungaji mkono mkubwa zaidi wa utawala wa Kizayuni wa Israel ambapo serikali ya Biden imetoa msaada mkubwa zaidi wa kijeshi na silaha kwa Tel Aviv wakati wa vita vya Gaza, ambavyo vimeingia katika mwezi wake wa saba.

Hali kadhalika Marekani ni muungaji mkono mkuu wa kisiasa wa Israel katika uga wa kimataifa ambapo imetumia mara kadhaa kura ya turufu katika baraza la Usalama kutetea utawala huo katili unaotekeleza mauaji ya kimbari huko Gaza. Lakini pamoja na uungaji mkono huo, kote Marekani, hasa katika vyuo vikuu kumeshuhudiwa ongezeko la upinzani mkali dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel unaotenda jinai.

Katika maandamano ya hivi karibuni ya kupinga uungaji mkono wa Washington kwa utawala wa Kizayuni kwa njia ya kuidhinisha msaada wa dola bilioni 26 za Marekani kwa utawala huo katika Baraza la Wawakilishi la Marekani na Baraza la Seneti la Marekani, baadhi ya wapinzani wa misaada kwa Israel wamefanya maandamano mbele ya makazi ya kiongozi wa Wademokrat katika Baraza la Wawakilishi la Marekani. Maandamano hayo ya amani yamegeuka kuwa ya vurugu na ghasia baada ya polisi kujaribu kuwatawanya waandamanaji. Katika vurumai hizo polisi waliwakamata waandamanaji wengi wanaopinga utawala wa kibaguzi wa Israel.

Wanafunzi na wahadhiri wa vyuo vikuu Marekani katika maandamano ya kupinga Israel

Hivi sasa zimepita zaidi ya siku  200 tangu kuanza vita vya Gaza na jinai zisizo na kikomo za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wasio na hatia wa Palestina kwa uungaji mkono wa kifedha, kijeshi na kisiasa wa serikali ya Biden. Kutokana na jinai hizo za Israell, vyuo vikuu vya Marekani vimekuwa uwanja wa ukandamizaji wa wanafunzi wanaoandamana. Katika kipindi cha miezi saba iliyopita, maandamano makubwa yamefanyika katika vyuo vikuu vya Marekani kupinga uhalifu wa Israel huko Gaza, hasa mauaji ya kimbari pamoja na kutumiwa vibaya njaa kama silaha ya kivita. Aidha wanafunzi hao wanataka hatua za haraka zichukuliwe kuushinikiza utawala katili wa Israel usitishe vita mara moja Gaza. Serikali ya Biden imekasirishwa sana na maandamano hayo ambayo yanafichua jinai za Israel na kwa msingi huo imechukua hatua za kuwakandamiza wanafunzi na wahadhiri wanaoshiriki katika mijumuiko dhidi ya Israel.

Kuhusiana na hili, polisi ya New York iitangaza Jumanne kwamba wanafunzi 133  wa Chuo Kikuu cha New York walikamatwa kwa tuhuma za  "uvurugaji nidhamu na kuimba nyimbo za vitisho na chuki dhidi ya Mayahudi."

Maandamano makubwa pia yamefanyika katika Chuo Kikuu cha Yale, Columbia na vyuo vikuu vingine mashuhuri Marekani kwa ajili ya kuonyesha mshikamano na Wapalestina wa Gaza na kulaani jinai za utawala wa Kizayuni. 

Ni jambo la kushangaza kwamba wanasiasa wa vyama vikuu vya Demokrat na Republican  wanapinga maandamano ya wanafunzi dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Trump

Katika muktadha huo, Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump amewaambia waandishi wa habari alipokuwa akienda mahakamani kwa siku ya sita ya kesi yake huko Manhattan alidai kuwa maandamano ya wanachuo wa Marekani dhidi ya Israel ni aibu.

Katika ngazi ya jamii ya Marekani, mielekeo ya kuukosoa utawala wa Kizayuni na kuwaunga mkono Wapalestina imezidi kushika kasi. Matokeo ya uchunguzi wa maoni ya Wall Street Journal, uliofanyika kuanzia tarehe 21 hadi 28 Februari, yanaonyesha kuwa wananchi wengi wa Marekani hawaridhishwi na utendaji wa Joe Biden katika vita vya Gaza na wanaamini kuwa utawala wa Kizayuni umetumia nguvu kupita kiasi kujibu operesheni ya Kimbunga cha Al Aqsa iliyotoekelezwa mnamo Oktoba 7.

Aidha katika uchunguzi mwingine wa nchi nzima uliofanyika mwishoni mwa Januari 2024 nchini Marekani, ilibainika kuwa nusu ya Wamarekani wanaamini kuwa utawala wa Kizayuni unafanya mauaji ya kimbari huko Gaza dhidi ya Wapalestina.

 

Tags