May 05, 2024 07:38 UTC
  • Ufaransa yamzuia daktari Muingereza aliyekuwa Gaza kuingia nchini humo kutoa ushahidi

Daktari mpasuaji mwenye uraia pacha wa Uingereza na Palestina, Ghassan Abu Sittah ambaye ni shahidi wa uhalifu wa kivita wa Israel katika Ukanda wa Gaza, amezuiwa kuingia Ufaransa, ambako alipangwa kuhutubia Baraza la Seneti kuhusu hali ya Gaza.

Daktari huyo amesema amezuiwa kuingia Ufaransa baada ya kufika katika uwanja wa ndege wa Charles De Gaulle kaskazini mwa Paris siku ya Jumamosi ya jana.

Abu-Sittah amesema aliambiwa kwamba Ujerumani ilikuwa imetekeleza marufuku ya Schengen ya kuingia katika nchi za Ulaya.
“Wananizuia kuingia Ufaransa. Ninapaswa kuzungumza katika Seneti ya Ufaransa leo," aliandika jana kwenye mtandao wa kijamii wa X.

Kaulimbiu ya mkutano huo ilikuwa; Ufaransa na wajibu wake wa kutekeleza sheria za kimataifa huko Gaza.

Mwezi uliopita pia mamlaka za Ujerumani zilimzuia daktari huyo bingwa kuingia Berlin, ambako Abu-Sitta alipangiwa kuhutubia mkutano ambako alialikwa kuzungumza juu ya kazi yake katika hospitali za Gaza.

Abu-Sittah alialikwa na wabunge wa chama cha Kijani kushiriki katika mkutano wa Sénat, baraza la juu la Ujerumani, kuzungumza juu ya mfumo wa huduma ya afya katika eneo lililozingirwa na jeshi la Israel la Gaza huko Palestina.

Taarifa ya kituo hicho imesema, "Wajerumani wananyamazisha shahidi mkuu wa uhalifu wa kivita wa Israel."

Gaza

Kituo cha Kimataifa cha Haki kwa Wapalestina (ICJP) - ambalo ni shirika huru la wanasheria, wanasiasa na wasomi - kimelaani kuzuiliwa kwa Abu-Sittah huko Paris na kuutaja kama "unyanyasaji usiokubalika wa mtaalamu wa matibabu anayeheshimika duniani."
Daktari huyo wa upasuaji alifanya kazi katika hospitali za Gaza za al-Shifa na al-Ahli Baptist miezi ya Oktoba na Novemba 2023. Katika siku zake 43 za kazi ya kujitolea, alisema alishuhudia "mauaji ya Israel dhidi ya raia."

Mwezi Januari mwaka huu ICJP ilikabidhi ushahidi kwa Scotland Yard kuhusu uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu uliofanywa na Israel huko Gaza, ikiwa ni pamoja na ushahidi kutoka kwa Abu-Sittah.