May 05, 2024 06:56 UTC
  • Safari ya Abdollahian Gambia kushiriki mkutano wa OIC wa kujadili changamoto za Waislamu hasa Palestina

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yupo Banjul, mji mkuu wa Gambia kwa ajili ya kushiriki katika mkutano wa 15 wa Wakuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, OIC.

 

Safari ya Amir Abdollahian nchini Gambia kushiriki katika mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, OIC.

Mkutano wa 15 wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamum, OIC umefanyika huko Gambia Jumamosi na Jumapili tarehe 4 na 5 Mei chini ya kaulimbiu ya 'Kuimarisha Umoja na Mshikamano Kupitia Mazungumzo ya Maendeleo Endelevu.' Masuala na changamoto mbalimbali za Ulimwengu wa Kiislamu hususan suala la Palestina na hali ya sasa ya Ukanda wa Gaza pia yamejadiliwa katika kikao hicho cha Banjul, Gambia. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo ni miongoni mwa waasisi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu pamoja na Morocco na Saudi Arabia imetumia kila fursa kusimamisha vita na kutoa misaada kwa wananchi wa Palestina wa Ukanda wa Gaza tangu kuanza mashambulizi ya kinyama yanayofanywa na utawala haramu wa Israel tokea mwezi Oktoba tarehe 7 mwaka jana. Mazungumza ya mara kwa mara kati ya maafisa wakuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hususan Rais na Waziri wa Mambo ya Nje katika miezi ya hivi karibuni na wenzao wa nchi nyingine kama vile Saudi Arabia, Uturuki, Qatar na Pakistan yanaweza kutathminiwa katika mtazamo huo. Hossein Amir Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, sambamba na kubainisha msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na matukio ya ulimwengu wa Kiislamu, eneo na kimataifa, amekutana na kujadiliana na baadhi ya viongozi wa nchi za Kiislamu pambizoni mwa mkutano huo. Katika mwendelezo wa kikao hicho cha wakuu wa nchi na wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, Achim Steiner, Mkurugenzi wa Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa UNDP ameelezea wasiwasi wake kuhusu maafa na uharibifu mkubwa unaosababishwa na mashambulizi ya Israel dhidi ya watu wa Gaza na kuongeza kuwa, ukarabati wa eneo hilo katika hali ya kawaida utachukua takriban miaka 80. Abdullah al-Dardari, Mkurugenzi wa Idara ya Ulimwengi wa Kiarabu ya Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa, pia amekadiria gharama ya kuijenga upya Gaza kuwa takriban dola bilioni 50 iwapo vita hivyo vitasimamishwa mara moja. Kwa mujibu wa takwimu za hivi punde, watu elfu 34, 622 wameuawa shahidi na wengine elfu 77, 867 wamejeruhiwa tangu kuanza kwa mashambulizi ya utawala ghasibu wa Israel katika Ukanda wa Gaza kuanzia tarehe 7 Oktoba mwaka jana, ambapo wengi wao wahanga wa mashambulizi hayo ni wanawake na watoto.  

Uharibifu mkubwa wa miundombinu ya Ukanda wa Gaza unaofanywa na utawala haramu wa Israel. 

Kwa maelezo hayo ni wazi kwamba ujenzi mpya na uungaji mkono kwa wakaazi wa Ukanda wa Gaza utawezekana tu kwa uhamasishaji mkubwa wa wananchi na uwekezaji wa nchi na taasisi za kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, OIC. Juhudi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na baadhi ya nchi pamoja na taasisi za kimataifa kwa ajili yya kusimamisha jinai za utawala wa Kizayuni huko ukanda wa Gaza, zinafanyika katika hali ambayo Wazayuni wanaoungwa mkono na chi za Marekani na Magharibi wanaendeleza jinai zao na sasa wanapanga njama za kuibua maafa mengine makubwa huko Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Baada ya kuwafukuza Wapalestina wapatao milioni moja na nusu katika maeneo tofauti ya Ukanda wa Gaza na kuwahamishia katika mji wa mpakani wa Rafah kusini mwa Gaza, sasa utawala haramu wa Kizayuni unapanga mipango ya kuushambulia mji huo kwa kizingizio cha kuwaangamiza wapiganaji wa Hamas katika eneo hilo.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu hususan Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa mwenyewe ametoa onya kali akisema kuwa iwapo mji wa Rafah utashambuliwa basi ulimwengu utashuhudia mauaji mengine makubwa zaidi ya Wapalestina huko Gaza.
Katika hali hiyo, Marekani na Uingereza zikiwa waungaji mkono wakubwa wa jinai na siasa za kujitanua utawala ghasibu wa Kizayuni katika eneo, badala ya kujaribu kusimamisha vita na mauaji ya utawala huo dhidi ya Wapalestina wa Gaza, zinaendelea kuwapa silaha Wazayuni na kupinga maazimio ya kusimamisha vita katika ukanda huo na hivyo kuwa washirika wakubwa wa mauaji ya kimbari yanayofanyika na utawala huo wa kibaguzi huko Gaza.

Bila shaka kipindi hiki kigumu kwa Wapalestina na eneo zima kitapita, lakini ni wazi kuwa namna kila nchi na mashirika ya kimataifa yalivyoamiliana na kuchukua msimamo kuhusu  mauaji haya ya wazi kabisa dhidi ya watu wasio na hatia, itasajiliwa katika historia.

Tags