May 06, 2024 12:10 UTC
  • Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu: Hija ya mwaka huu ni Hija ya kujitenga na adui Mzayuni na waungaji mkono wake

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kwa kuzingatia Aya za Qur'ani Tukufu na kumbukumbu ya jina lililobarikiwa la Nabii Ibrahim (AS), ibada ya Hija ya mwaka huu inapaswa kuwa zaidi ya Hija ya kila mwaka, na inabidi iwe Hija na kutangaza kujitenga na adui wa Waislamu, Mzayuni mtenda uhalifu na wafuasi wake.

Ayatullah Ali Khamenei ambaye mapema leo alihutubia kikao cha maafisa na wasimamizi wa msafara wa mahujaji wa Iran wanaoelekea katika ardhi tukufu kwa ajili ya ibada ya Hija, ameashiria jinai zinazofanywa na utawala unaofyonza damu wa Israel huko Gaza na kusema: Matukio ya sasa ya Gaza ni kiashiria cha kudumu cha historia. Ameongeza kuwa: Mashambulizi ya kikatili ya jibwa kichaa la Kizayuni kwa upande mmoja, na mapambano na kudhulumiwa kwa watu wa Gaza, kwa upande mwingine, vitabakia katika historia na kuwaonyesha njia wanaadamu; na hapana shaka kuwa kuakisiwa kusiko na kifani kwa ukatili na mapambano hayo katika jamii zisizo za Kiislamu na vyuo vikuu nchini Marekani na katika baadhi ya nchi nyingine ni miongoni mwa viashiria hivyo vya kihistoria. 

 Akieleza wajibu wa Umma wa Kiislamu kuhusiana na maafa ya Gaza katika Hija ya mwaka huu, Ayatullah Khamenei ameashiria mifano kadhaa iliyotajwa katika Qur'ani Tukufu na sira ya Nabii Ibrahim (as). Amesema: Ibrahim (as) ni miongoni mwa Mitume waliokuwa na moyo wa ukarimu na mwema, lakini nabii huyu huyu wa Mwenyezi Mungu alitangaza kujibari na kujitenga na maadui wakatili.

Viongozi wa msafara wa Hija wa Iran

Akigusia Aya za Qur'ani zinazokataza kikamilifu kufanya urafiki na maadui madhalimu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa ni kielelezo tosha cha uadui dhidi ya Waislamu, na Marekani kuwa ni mshirika wa utawala huo. Ayatullah Khamenei amehoji kwamba, lau isingelikuwa msaada wa Marekani, je utawala wa Kizayuni ungekuwa na nguvu na ujasiri wa kuwatendea unyama Waislamu, wanawake na watoto?

Ayatullah Khamenei amesema: Wauaji wa Waislamu wanaowafurusha makwao na waungaji mkono wao, wote wawili ni madhalimu, na kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu, mtu akifanya urafiki nao, yeye pia ni dhalimu na hupatwa na laana ya Mwenyezi Mungu.

Amesema kwa kuzingatia hali ya hivi sasa ya Ulimwengu wa Kiislamu, kuna udharura zaidi wakati huu kutekelezwa Hija ya Kiibrahim kuliko wakati wowote mwingine, yaani, kutangaza hasira na chuki dhidi ya maadui; Kwa kuzingatia hayo, mahujaji wa Iran na wasio Wairani wanapaswa kufikisha mantiki ya Qur'ani ya kuliunga mkono taifa la Palestina kwa ulimwengu mzima wa Kiislamu.