May 19, 2024 02:48 UTC
  • OCHA: Kwa kuzuiwa uingizaji misaada, hakuna kilichobaki kugawa katika Ukanda wa Ghaza

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imeonya dhidi ya kuzuiwa uingizaji misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Ghaza na kutangaza kuwa hakuna kilichosalia kwa ajili ya kuwagaia Wapalestina wa eneo hilo.

OCHA imeeleza kwenye ujumbe ilioweka kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X: "hali ya maji na majitaka katika Ukanda wa Ghaza inazidi kuzorota kwa kasi, na kutokana na kupigwa marufuku uingizaji misaada ya kibinadamu katika eneo hili watu wanaweza tu kukidhi mahitaji yao kwa kutafuta chakula na mahitaji mengine chini ya vifusi na kwenye mabaki ya takataka".

Farhan Haq

Kabla ya hapo, Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa alieleza kuhusu hali ya Ghaza kwamba, Ofisi ya Uratibu Masuala wa Masuala Kibinadamu (OCHA) inasema, vivuko vya kusini mwa Ghaza vimefungwa kwa siku kadhaa sasa, hakuna usalama wa kuvifikia na hali ya huduma za kilojistiki haiwezi kudumu kwa muda mrefu.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa aliongeza pia kuwa, OCHA imebainisha kwamba hali katika Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na eneo la mashariki mwa Baitul Muqaddas, ingali ni ya kutia wasiwasi kutokana na kuendelea machafuko na ukandamizaji unaofanywa na wanajeshi wa Israel pamoja na walowezi, uharibifu wa mali za raia na kuongezeka watu wanaolazimishwa kuhama makazi yao.

Kuhusiana na hilo, msemaji wa OCHA Jens Laerke, alitangaza wiki iliyopita wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, kwamba wakati Ukanda wa Ghaza unakaribia kuzama kikamilifu kwenye lindi la baa la njaa, utawala wa Israel unazuia misafara ya chakula kuingia katika eneo hilo.

Aidha, Laerke aliwaambia waandishi wa habari kwamba kuzuiwa uingiaji wa misafara ya chakula ambayo ilipasa kuelekezwa hasa kaskazini mwa Ghaza, ambako asilimia 70 ya watu walioko huko wanakabiliwa na janga la njaa, unafanywa kwa ugumu mara tatu zaidi kuliko uzuiaji wa misafara iliyobeba misaada ya kibinadamu.

Mnamo Mei 7, jeshi la utawala wa Kizayuni lilifanya uvamizi na shambulio la nchi kavu dhidi ya mji wa Rafah ulioko kusini mwa Ukanda wa Ghaza na kukifunga kivuko cha mji huo cha baina ya Ghaza na Misri, ambacho kinachukuliwa kuwa moja ya njia muhimu zaidi za kupitishia misaada ya kibinadamu kuelekea eneo hilo la Palestina.

Operesheni hiyo ya uvamizi ilianza saa chache tu baada ya harakati ya Hamas kutangaza kwamba imekubali pendekezo la kusitisha mapigano lililotolewa na Misri na Qatar, pendekezo ambalo utawala wa Kizayuni ulilikataa.../

 

Tags